1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vipi raia wa Afrika Kusini alivyoshuhudia kuanguka kwa ukuta

Samia Othman3 Novemba 2009

<p>Ukumbusho wa hali ya maisha ilivyokuwa katika ile iliokuwa (GDR)-Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani au Ujerumani Mashariki, ni mada ya kutatanisha.

https://p.dw.com/p/KL4G
Ukuta wa Berlin
Nadra maoni kuwa ya upande mmoja tu -mazuri au mabaya.Hali pia iko hivyo kwa wakaazi wa kigeni walioishi huko wakati ule hadi Novemba 9,1989-miaka 20 iliopita pale ukuta wa Berlin ulipoanguka.

Hali kama hiyo ya kutoweza kusema maisha yalikuwa ama mabaya au mazuri tu, inamkumba pia Eric Singh.Akiwa amezaliwa, 1932 huko Durban,Afrika Kusini,Eric Singh, alitafuta ukimbizi katika Ujerumani Mashariki ili kujikinga na mkandamizo na dhulma iliopita wakati ule nchini mwake.

Kutoka ardhi ya berlin Mashariki,Eric Singh, mkereketwa wa chama cha ANC,aliongoza mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi na katika vita hivyo alipewa msaada tangu wa kisiasa hata wa fedha na serikali ya Ujerumani mashariki (GDR).

Hata baada ya kuporomoka ukuta ,Eric Singh amebakia Berlin .

Aliulizwa maoni yake huko Afrika Haus-jumba la Afrika , jinsi anavyoikumbuka Jamhuri ya kidemokrasi ya Ujerumani ?

Je, mkutano mmoja na waandishi habari waweza kuibadili dunia ? Kwa maoni ya mwandishi habari ambaye Novemba 9, 1989 aliekuwepo katika mkutano huo na msemaji wa serikali ya Ujerumani mashariki Günther Schabowski,jawabu ni ndio waweza.

Kwani katika mkutano huo ,ndipo hatima ya ukuta wa Berlin ilipokatwa muda mfupi kabla saa 1 ya usiku kugonga.Günther Schabowski alinadi mbele ya kamera za maripota wa ndani na wa nje ya Ujerumani,ni ruhusa hapo hapo kwa raia wa Ujerumani Mashariki kusafiri nje . Eric Singh, alikuwepo hapo. Mwafrika Kusini huyo akiishi Berlin na akiripoti kwa magazeti mbali mbali kutoka Berlin.Anaamini kwa hivyo, alikuwepo wakati historia ikiandikwa. Anasema;

"Niliusikiliza kwa makini mkutano ule na waandishi habari. Nikalisikia suali aliloulizwa Riccardo,Riccardo Ehrmann-mwandishi kutoka Itali.Aliuliza swali hili: Lini mipaka itafunguliwa ?Pale Bw.Schabowski alipojibu.... ni leo hii,hapo zikaanza pirika pirika za kuhama."

Muda mfupi baada ya mkutano huo na waandishi habari ulioonekana pia katika TV ya Taifa ,wananchi wa kwanza wa Ujerumani Mashariki wakaanza kumiminika vituoni mjini humo ili kuvuka mpaka .Walinzi wa mpakani walioelemewa na wimbi la watu ,wakawaachia watu kuelekea upande wa pili wa mpaka ambao ulikuwa marufuku kwenda.Taarifa za kuweza kuondoka nchini zilipozagaa ,umma mkubwa zaidi ukamiminikia kituo cha mpakani cha Berlin mashariki kuujaribu uhuru wao waliopata.

Ilipoingia usiku wa manane ,mipaka yote ilikuwa wazi.Mpaka wa Berlin ukawa hadithi iliopita. Hali hiyo, alijionea binafsi Eric Singh kutoka Afrika Kusini kama mkaazi siku ya pili yake.Kwani, Novemba 10,alipanda treni " S-Bahn" kutoka barabara ya Friederichstrasse kuelekea nae Berlin Magharibi.

Alisimulia alipofika Friederichstrasse, kulikuwapo umati wa watu na hasa vijana.Halafu wakavuka mto Spree hadi Berlin magharibi."Sote tulishangiria kwa kupiga makofi"-alisema Singh akiongeza," niliweza kuwaelewa vizuri kwa vile, mwishoe nao, waliweza kusafiri nje ya nchi yao.Kwani, nikiwa mpiganaji-wa ukombozi,hata nami sikuruhusiwa kusafiri nje ya Afrika Kusini.Sikupewa paspoti ya kusafiria."

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Abdul-Rahman