Vita Sudan Kusini vyafikia kiwango kibaya
15 Februari 2017Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema kwenye ripoti iliyopatikana na Shirika la habari la la Ufaransa AFP Jumanne kwamba, wananchi wanatoroka vijiji na miji yao kwa idadi kubwa na kwamba kuna hatari ya mauaji ya kiasi kikubwa.
Onyo hilo linafuatia msururu wa mikutano aliyoifanya Guterres na viongozi wa kanda hiyo pamoja na rais wa Sudan Kusini Salvar Kiir mwezi uliopita, ili kutilia kikomo mapigano hayo ya miaka mitatu.
"Hali ya usalama inaendelea kudorora katika baadhi ya maeneo nchini humo na matokeo ni kwamba machafuko haya yanayoendelea yamefikia kiwango kibaya kwa wananchi," aliandika Guterres.
Operesheni za kijeshi zilizofanywa na pande zote na hasa vikosi vinavyomuunga mkono rais Kiir, zilikuwa zinaharibu nyumba kila siku, ilisema ripoti hiyo iliyotumwa kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu.
Huenda serikali ikashindwa kudhibiti makundi ya wanamgambo
"Ongezeko la wanamgambo chini ya uongozi dhaifu wa SPLA ama makamanda waasi, ni hatari kwani iwapo mkondo huu utaendelea huenda serikali ikashindwa kuudhibiti kwa miaka mingi ijayo," ilisema ripoti hiyo.
Guterres amekuwa akiwataka viongozi wa kanda hiyo kama rais wa Uganda Yoweri Museveni, aliye karibu na Kiir, kumshinikiza kiongozi huyo wa Sudan Kusini kuongoza vikosi vyake na kujiondoa kutoka kwenye mapigano.
Umoja wa Mataifa una vikosi 13,000 vya kulinda amani nchini Sudan Kusini, lakini vikosi hivyo vimezuiwa na majeshi ya serikali na waasi kufika maeneo ambayo mapigano yanafanyika.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba wiki iliyopita mwanajeshi wa kulinda amani aliyekuwa kwenye doria katika eneo la Ikweta mashariki, alisimamishwa na wanajeshi 4, akatolewa nje ya gari lake na kupigwa.
Mataifa kadhaa kutuma wanajeshi
Kufuatia mkutano wake na Kiir, Guterres amesema kuna hatua ambazo zimepigwa katika kutuma kikosi cha kanda hiyo kilicho chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa, ili kuimarisha usalama katika mji mkuu Juba.
Rwanda inatarajiwa kutuma vikosi na helikopta katika awamu ya kwanza inayotarajiwa kuwa mwezi Machi ama Aprili, nayo Ethiopia inajitayarisha kutoa mchango wake wa wanajeshi.
Ripoti hiyo inazidi kueleza kwamba Kenya bado haijaandaa mazungumzo kuhusu kutoa mchango wake kwa kikosi hicho cha wanajeshi 4,000 na mzozo uliopo kuhusiana na uwepo wa vikosi hivyo katika uwanja wa ndege wa Juba, bado haujapatiwa suluhu.
Baada ya kuamua kujitenga na Sudan na kuwa huru mwaka wa 2011, Sudan Kusini ilitumbukia kwenye mapigano mwaka wa 2013, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na zaidi ya wengine milioni 3 kutoroka nchi hiyo, wakikimbilia nchi jirani za Uganda na Kenya .
Mwandishi: Jacob Safari/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman