Vyombo vya usalama DRC vinazuwia uchunguzi
2 Mei 2018Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma wachunguzi wa Umoja huo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kusaidia maafisa nchini humo kuwabaini watu waliohusika katika mauaji mwaka jana ya Mmarekani Michael Sharp na Zaida Catalan raia wa Sweden katika jimbo la Kasai.
Ikiongozwa na Robert Petit kutoka Canada, timu hiyo imekuwa ikifanyakazi tangu mwezi Novemba na mwendesha mashitaka wa jeshi la Congo katika mji wa Kananga katika jimbo la Kasai, lakini mafanikio yamekuwa madogo, imesema ripoti hiyo iliyotumwa katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki mbili zilizopita.
Mwezi Agosti, uchunguzi wa Umoja wa mataifa uiligundua kwamba wanamgambo wa eneo hilo huenda wanahusika katika mauaji ya watu hao wawili waliokuwa wakifanya uchunguzi wa machafuko katika eneo hilo kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo.
Sharp na Catalan walikuwa wakifanya uchunguzi kuhusiana na makaburi yaliyozikwa watu wengi na uhalifu ulioambatana na uasi katika jimbo la Kasai ambako walitekwa pamoja na wenzao raia wa Congo Machi mwaka 2017.
Miili ya Sharp, mratibu wa kundi hilo na mtaalamu wa silaha, na Catalan , ambaye alikuwa mtaalamu wa masuala ya kiutu, iligunduliwa katika kaburi na wanajeshi wa kulinda amani wiki kadhaa baada ya kutoweka. Catalan alikatwakatwa.
Watuhumiwa wahamishwa
Baada ya kukamatwa kwa wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi la wanamgambo, Vincent Manga na Francois Badibanga, mwezi Machi, uchunguzi wa Umoja wa Mataifa uliweza kwa muda mfupi kuwahoji mjini Kananga kabla ya ghafla kuhamishwa kwenda Kinshasa, "wakiwa katika mahabusu ya jeshi la polisi," ripoti hiyo imesema.
Timu ya Umoja wa Mataifa inataka kumhoji mkalimani ambaye alikuwa ameongozana na wataalamu hao waliouwawa, Thomas Nkashama, lakini "duru kadhaa za kuaminika zimemuweka mtu huyo mikononi mwa polisi kwa muda," ripoti imeeleza.
"Ni wazi kabisa kwamba vyombo vya usalama mjini Kinshasa vinaendelea kuingilia kati na hatua za mahakama na vinadhibiti njia ya kuwapata mashahidi muhimu na watuhumiwa," imesema ripoti hiyo iliyotayarishwa na idara ya masuala ya kisiasa ya Umoja wa mataifa.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamewaomba maafisa wa Congo ruhusa ya kuwahoji watuhumiwa wanne wengine waliokamatwa mwezi Desemba na kuwekwa kizuwizini mjini Kinshasa, lakini kwa sasa wanasubiriwa kupelekwa mjini Kananga licha ya uhakikisho kutoka waziri wa sheria. Jumla ya watuhumiwa 26 wanakabiliwa na mashitaka kwa mauaji ya Sharp na Catalan, 14 kati yao wanashitakiwa wakiwa hawapo mahakamani, lakini ripoti hiyo imeeleza kuwapo na matundui kadhaa katika kesi hiyo iliyowasilishwa na mwendesha mashitaka.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman