1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji 26 wauawa DRC

21 Desemba 2016

Waandamanaji 26 wameuawa na wengine kadhaa kukamatwa kwenye maandamano ya kumpinga Rais Joseph Kabila kuendelea kubakia madarakani hata baada ya muda wake kumalizika kikatiba katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/2Uen0
Demokratische Republik Kongo Proteste gegen Kabila
Picha: Reuters/T. Mukoya

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch linasema wanajeshi na maafisa wa polisi walirusha risasi ovyo ovyo kwa waandamanaji, jambo linalozusha wasiwasi kwamba huenda watu wengi zaidi wameuawa katika siku ya kwanza baada ya muda wa Kabila kumalizika.

Mtafiti wa shirika hilo, Ida Sawyer, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba mauaji ya siku ya Jumanne (Disemba 20) yalifanyika kwenye mji mkuu, Kinshasa, mji wa kusini wa Lubumbashi na maeneo mengineyo. Wakaazi walisema kikosi maalum cha rais, Republican Guard, kilikuwa kikipita nyumba kwa nyumba kuwasaka na kuwakamata vijana.

Mjini Kinshasa, waandamanaji waliyachoma moto makao makuu ya chama tawala. Serikali inasema watu tisa waliuawa mjini humo, akiwemo "afisa mmoja wa polisi, wanawake wawili waliopigwa risasi kwa bahati mbaya na vijana sita waliokuwa wakiiba madukani."

Katika kitongoji cha Matonge, watu walijitokeza kucheza mpira barabarani kuzuwia magari yasipite kama aina moja ya kuandamana, huku kukiwa na kiwango kikubwa cha wanajeshi na polisi mitaani.

"Kabila ameisaliti nchi yetu. Lazima aondoke," alisema Jean-Marcel Tshikuku, fundi gereji, akiongeza kwamba: "Alitangaza serikali mpya mwisho wa muhula wake. Ni matusi. Hatumtaki tena. Hatutaki mazungumzo. Tunataka aende. Aondoke tu!"

Juhudi za kusaka maridhiano

Kongo Präsident Joseph Kabila
Kwa mujibu wa katiba ya Kongo, muda wa Rais Joseph Kabila kubakia madarakani ulimalizika tarehe 20 Disemba 2016 na haruhusiwi kuwania muhula mwengine.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Mazungumzo ya kusaka muafaka wa kisiasa kati ya chama tawala na upinzani yalikwamba mwishoni mwa wiki na kutazamiwa kurejea tena Jumatano, chini ya upatanishi wa Kanisa Katoliki.

Marekani imesema imefadhaishwa sana "na kushindwa kwa Rais Kabila kuandaa uchaguzi na kuelezea waziwazi kwamba hatogombea tena." Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, John Kirby, aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba nchi yake inalaazi ghasia za hivi karibuni na kutoa wito kwa pande zote kushiriki kwenye mazungumzo ya Jumatano "kwa ukamilifu na nia njema."

Kabila, aliyeingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake, anazuiwa kikatiba kuwania muhula mwengine, lakini mahakama iliamua kwamba anaweza kubakia madarakani hadi uchaguzi mwengine, ambao umeahirishwa kwa kipindi kisichofahamika. Awali ulikuwa ufanyike mwezi Novemba, lakini baadaye chama tawala kilisema kinahitaji angalau mpaka mwezi Aprili 2018.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Etienne Tshisekedi, ametoa wito wa kutumia njia za amani kupingana na kile anachokiita "mapinduzi ya Kabila". Katika ujumbe aliotuma kupitia mtandao wa YouTube, mwanasiasa huyo mkongwe alikiita kitendo cha Kabila kuwa ni "uhaini", huku akiwataka raia wa Kongo na jumuiya ya kimataifa kutokuutambua tena utawala wa Kabila.

Matakwa ya wapinzani

Kinshasa Samy Badibanga Pressekonferenz
Muda mchache kabla ya kumalizika kwa muda wa Rais Joseph Kabila, Waziri Mkuu Samy Badibanga alitangaza serikali mpya ya mpito.Picha: Reuters/K.Katombe

Mkwamo huo wa kisiasa umeongeza khofu ya kuenea kwa machafuko katika taifa hilo kubwa katikati ya Afrika, ambalo licha ya kuwa na madini yenye thamani ya trilioni za dola, bado ni miongoni mwa mataifa fukara kabisa na moja ya mataifa yasiyokuwa na utulivu wa kisiasa.

Wakati mazungumzo yalipositishwa mwishoni mwa wiki iliyopita, yalikuwa yameshindwa kufikia makubaliano juu ya tarehe ya uchaguzi mpya au kuwachiwa kwa wafungwa wa kisiasa. Mambo hayo mawili ni miongoni mwa matakwa muhimu ya wapinzani, sambamba na kufutwa kwa mashitaka ya uhalifu dhidi ya kiongozi wa upinzani, Moise Katumbi, ambaye aliikimbia nchi yake wakati mamlaka zilipotangaza mipango ya kumshitaki. 

Wafuasi wa Katumbi wanasema mashitaka ya kukodi mamluki ni ya kisiasa, kwa kuwa alikuwa mgombea urais anayeongoza.

Serikali ya Kabila imekuwa ikijaribu kutuliza mtafaruku wa kisiasa kwa kuwashirikisha baadhi ya wapinzani kwenye uongozi. Muda mfupi kabla ya muda wa Kabila kumalizika, Waziri Mkuu mpya, Sami Badibanga, alitangaza serikali mpya ya mpito. 

Badibanga mwenyewe alikuwa sehemu ya wapinzani wasiokuwa na ushawishi mkubwa kwa umma, ambao walishiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika na kusainiwa mwezi Oktoba. Hata hivyo, mazungumzo hayo yaligomewa na sehemu kubwa ya wapinzani wenye nguvu, akiwemo Tshisekedi.

Ndani na nje ya Kongo, watu wanahofia kurejewa kwa mauaji ya mwezi Septemba, pale wapinzani walipomiminika mitaani baada ya tume ya uchaguzi kushindwa kutangaza tarehe ya uchaguzi wa rais.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga