Waandamanaji Sudan wadai utawala wa kiraia haraka
14 Aprili 2019Waandamanaji wamedai kuundwa serikali ya kiraia haraka iwezekanavyo na bila masharti ambayo itatawala kwa muda wa miaka minne.
Vyama vya kisiasa na vuguvugu lililokuwa nyuma ya miezi minne ya maandamano vimesema katika taarifa ya pamoja jana Jumamosi (13.04.2019) kwamba watabaki mitaani hadi pale madai yao yatakapofikiwa. Wamesema hatua ya kukabidhi madaraka katika serikali ya kiraia itakuwa hatua ya kwanza kuelekea katika kuanguka kwa utawala.
Jeshi limeteua baraza la kijeshi ambalo inasema litatawala kwa miaka miwili ama pungufu wakati uchaguzi ukitayarishwa. Baraza hilo lilikutana na ujumbe wa watayarishaji wa maandamano jana Jumamosi.
Jeshi lilimpindua al-Bashir siku ya Alhamis, na kufikisha mwisho karibu miaka 30 ya utawala wake na kumuweka chini ya kizuwizi cha nyumbani kwake katika mji mkuu Khartoum. Waandamanaji wanahofu kwamba jeshi , ambalo linadhibitiwa na wateule wa al-Bashir, litang'angania madarakani ama kumchagua mmoja kati yao kumrithi.
Saudi Arabia na Umoja wa falme za Kiarabu wakati huo huo zimetoa taarifa kuunga mkono baraza la keshi la mpito nchini. saudi Arabia imesema "inasimama pamoja na watu wa Sudan" na kutoa wito kwa wasudan wote "kutoa umuhimu kwa maslahi ya kitaifa" kwa nchi yao.
Umoja wa Falme za Kiarabu UEA , imewataka wasudan "kufanyakazi kwa ajili ya kulinda uhalali na kuhakikisha mabadiliko ya amani ya madaraka."
Mfalme wa saudia Salman ameamuru kiasi ambacho hakikutajwa cha misaada kwa Sudan ambayo ni pamoja na bidhaa za mafuta ya petroli , ngano na madawa.
Katika taarifa nyingine tofauti iliyotolewa jioni ya jana Jumamosi, Saudi Arabia na UAE hususan zilielezea uungaji wao mkono wa baraza la mpito la Sudan lililoundwa na jeshi.
Amri ya hali ya hatari
UAE imesema inakaribisha kuapishwa kwa jenerali Abdel - Fattah Burhan siku ya Ijumaa kuwa mkuu wa baraza hilo.
Burhan amechukua uongozi wa baraza la kijeshi siku moja baada ya kuondolewa kwa al-Bashir baada ya waandamanaji kupinga baraza hilo kuongozwa na jenerali Awad ibn Ouf, ambaye anaonekana kuwa yuko karibu sana na al-Bashir.
Katika matamshi yaliyotangazwa katika televisheni ya taifa , Burhan alisema Jumamosi baraza limewaalika "makundi yote ya Wasudan katika majadiliano."
Amesema anaondoa amri ya kutotembea usiku iliyowekwa siku ya Alhamis, ambayo ilikuwa idumu kwa muda wa mwezi mmoja, na kutangaza kuachiwa mara moja kwa wale waliokamatwa na kuwekwa kizuwizini na kufikishwa mahakamani chini ya wimbi la machafuko ambayo yalianza Desemba mwaka jana.
Al-Bashir aliweka amri ya hali ya hatari mwezi Februari, akipiga marufuku mikusanyiko ambayo haikuidhinishwa na kutoa madaraka makubwa kwa polisi katika juhudi za kuzima maandamano. Dazeni kadha za watu waliuwawa katika mapambano kati ya polisi na waandamanaji, na mamia wamehukumiwa katika mahakama za dharura.
Waandamanaji wamelielekeza vuguvugu lao katika mapinduzi ya umma ya mataifa ya Kiarabu ya mwaka 2011 ambayo yamewaondoa viongozi kutoka madarakani nchini Misri, Tunisia, Libya na Yemen. Wamechukua nyingi ya nyimbo na kauli mbiu, na kuchukua hatua za kukaa nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum mapema mwezi huu.
Mapinduzi ya aina hiyo yameacha mchanganyiko wa hali halisi, ambapo ni Tunisia pekee iliyojitokeza kuwa na utawala wa kidemokrasia.