1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroHaiti

Waandishi wa habari wauawa na genge la wahalifu Haiti

25 Desemba 2024

Waandishi wawili wa habari waliokuwa wakiripoti kwenye hafla ya kufunguliwa tena kwa hospitali ya rufaa ya chuo kikuu cha Haiti katika mji mkuu Port-au-Prince, wameuawa baada ya kushambuliwa na genge la wahalifu.

https://p.dw.com/p/4oZJN
Haiti I Mke wa mwandishi wa habari aliyepigwa risasi wakati wa shambulio hilo
Mke wa mwandishi wa habari aliyepigwa risasi wakati wa shambulio la genge la wahalifu huko Port-au-Prince, Haiti.Picha: Odelyn Joseph/AP/picture-alliance

Taarifa zaidi zinafahamisha kwamba waandishi wengine wa Habari waliojeruhiwa katika tukio hilo wanapokea matibabu katika hospitali nyengine.

Hospitali hiyo ya chuo kikuu ambayo ni Hospitali Kuu ya Haiti, ilikuwa imefungwa tangu mwezi Februari baada ya kushambuliwa na genge hilo la wahalifu. Shuhuda wa tukio hilo amelieleza shirika la habari la AFP kuwa watu kadhaa wamejeruhiwa, ingawa idadi kamili bado haijulikani.

Soma pia: UN: Watu 184 wafariki dunia Haiti kutokana na ghasia

Hali ya kiusalama bado ni tete nchini Haiti. Ujumbe wa kimataifa wa kuwasaidia polisi wa Haiti unaoongozwa na Kenya, umekuwa na mafanikio kidogo kutokana na kuendelea kwa ghasia za makundi yenye silaha ambayo yanashutumiwa kufanya mauaji, ubakaji, uporaji na utekaji nyara.