1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi wa kikanda waidhinisha uchaguzi wa DRC

2 Januari 2019

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamesema uchaguzi wa rais nchini DRC ulikwenda vizuri.

https://p.dw.com/p/3Aw0i
Wahlen im Kongo
Picha: Reuters/B. Ratner

Uidhinishwaji huo wa tahadhari kutoka jumuiya ya SADC unakinzana na madai ya wagombea wa upinzani kwamba uchaguzi huo wa Desemba 30 ulikumbwa na kasoro kadhaa na ukosoaji kutoka kwa mbunge mwandamizi wa Marekani kwamba uchaguzi huo "haukuwa huru wala wa haki."

Kuidhinishwa kwa matokeo ya uchaguzi na mataifa makubwa wanachama wa SADC kama vile Afrika Kusini na Angola kutakuwa muhimu kwa uhalali wa utawala wa rais ajaye, atakayerithi mikoba ya rais wa sasa Joseph Kabila hapo Januari 18.

Angola na Afrika Kusini zimekuwa washirika muhimu wa Kabila kwa miaka kadhaa, lakini uhusiano uliingia doa kwa kukataa kwake kuachia madaraka baada ya kumalizika rasmi kwa muhula wake mwaka 2016.

Logo von SADC
Kuidhinishwa kwa uchaguzi na mataifa makubwa ya SADC - Afrika Kusini na Angola - ni muhimu kwa uhalali wa utawala wa rais ajaye nchini DRC.

Uchunguzi wa maoni kabla ya uchaguzi ulionyesha kuwa mgombea anayependelewa na Kabila, waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Emmanuel Ramazani Shadary, alikuwa akishika mkia nyuma ya wagombea wakuu wa upinzani, Martin Fayulu na Felix Tshisekedi, lakini pande zote mbili zinasema zinatarajia kushinda. Matokeo ya awali yanatarajiwa Januari 6, na matokeo ya mwisho yatatolewa Januari 15.

Uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumapili ulinuiwa kuiongoza Congo kuelekea mabadilishano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia tangu nchi hiyo ilipopata uhuru miaka 59 iliyopita. Lakini zaidi ya Wacongo milioni moja katika ngome za upinzani walizuiwa kupiga kura kutokana na mripuko wa ugonjwa wa Ebola, migogoro ya ndani na matatizo mbalimbali ya usafirishaji.

Sehemu kubwa ya raia walitekeleza haki yao

"Kwa kuzingatia changamoto kadhaa zilizoukumba uchaguzi huu, (ujumbe wetu) umebaini kuwa uchaguzi...ulisimamiwa vizuri kwa kiasi," ulisema ujumbe wa SADC katika taarifa hiyo. Uchaguzi uliruhusu "Wacongo walio wengi kutimiza haki yao ya kupiga kura."

Taarifa hiyo ilisema asilimia 59 ya maeneo ya kupigia kura walioshuhudia yalifunguliwa kwa wakati, shughuli ya kuhesabu kura ilifanyika kwa uwazi na askari polisi waliokuwa wanalinda uchaguzi huo walifanya kazi yao kwa ueledi.

Demokratische Republik Kongo Wahlmaschine
Waangalizi wa SADC wamesema sehemu kubwa ya wapigakura walitekeleza haki yao na hilo ni muhimu katika mchakato wa uchaguzi.Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Ujumbe wa uangalizi kutoka Umja wa Afrika ulisema katika taarifa tofauti siku ya Jumatano, kwamba siku ya uchaguzi, ambayo pia ilihusisha uchaguzi wa wabunge wa bunge la taifa na mabunge ya majimbo, ilipita kwa amani, ingawa kulikuwa na changamoto kadha wa kadha za usafirishaji.

"Kufanyika kwa uchaguzi huu kunaashiria ushindi mkubwa kwa watu wa Congo," ulisema ujumbe huo. "Ujumbe unashauku kubwa kwamba matokeo yatakayotangazwa yanawiana na kile walichokipigia kura Wacongo."

Serikali ya Kabila ilikataa kuwaidhinisha waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya na kituo cha Carter chenye makao yake nchini Marekani, ambacho kilisema kulikuwa na kasoro nyingi katika uchaguzi wa mwaka 2011.

Matokeo ya uchaguzi yaliyobishaniwa ya mwaka 2006 na 2011 yalisababisha maandamano ya vurugu ya mitaani, na mgogoro wowote mara hii unaweza kuyavuruga maeneo tete ya mpakani mwa Congo na Rwanda, Uganda na Burundi, ambako makundi kadhaa ya wapiganaji yanaendesha shughuli zao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Josephat Charo