Waangalizi waridhika na maandalizi ya uchaguzi
3 Machi 2013Katika kikao na waandishi wa habari, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Mataifa ya Afrika, AU, Bi Nkosazana Dlamini Zuma amesema kuwa ujumbe wake umekutana na Rais Mwai Kibaki na kuwahakikishia kuwa shughuli za uchaguzi zitafanywa kwa njia ya amani.
Aidha kiongozi huyo alikutana pia na viongozi wa vyama mbalimbali, maafisa wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka na pia Inspekta Mkuu wa Jeshi la Polisi ambao wote walimwelezea kuridhika kwao na matayarisho ya uchaguzi.
"Wakenya wako tayari kwenda kwenye uchaguzi mnamo Jumatatu na ujumbe wetu umekutana na baadhi ya wagombea wa kiti cha Urais na wako tayari kupiga kura kwa amani na kukubali matokeo".
Bi Zuma aliandamana na aliyekuwa Rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano, ambaye ni kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa ya Afrika. Alisema kulikuweko na hali ya taharuki katika maeneo kadha nchini kufuatia uvumi kuwa baadhi ya watu walikuwa wanasambaza vikaratasi kwa nia ya kueneza chuki, japo walipewa hakikisho kuwa suala hili lilikwisha dhibitiwa na polisi. Chisano anahimiza wagombea wazingatie imani walionayo kwa katiba na kuwasilisha malalamiko yote kortini.
"Bi Dlamini ametoa mwito kwa Wakenya kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumatatu ili kumchagua kiongozi wampendaye.
Wakati huo huo amewahimiza wale wanaowania viti vya uongozi waitikie uamuzi wa wananchi".
"Washindi waitikie ushindi kwa unyenyekevu na kwa wale watakao shindwa wakumbuke kwamba bado wanahitajika katika ujenzi wa taifa.Tunatumai mambo yatakuwa shwari".
Zaidi ya waangalizi wapatao 20,000 kutoka makundi mbali mbali, miongoni mwao wale kutoka Jumuiya ya Ulaya, Umoja wa Kiafrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki wamo nchini Kenya kwa shughuli ya hii muhimu.
Mwandishi: Reuben Kyama / DW correspondent/ Nairobi
Mhariri : Sekione Kitojo