Waangalizi wawataka Wakenya kuwa na subira
7 Machi 2013Tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC, imerejelea shughuli ya kujumlisha matokeo ya kura kutoka majimbo yote 291 ya uchaguzi kote nchini baada ya mfumo wa uwasilishaji matokeo hayo kwa njia ya elektroniki kukwama siku moja baada ya kukamilika kwa uchaguzi.
Huku shughuli ya ujumuishaji matokeo ikiendelea katika kituo cha taifa cha ujumlishaji matokeo ya uchaguzi mkuu, miito mbali mbali inaendelea kutolewa kwa Wakenya kuzidi kuendelea na utulivu ili kudumisha amani. Ujumbe wa waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya umesema umeridhishwa na jinsi wakenya walivyopiga kura kwa amani na kuwarai kuendelea kuvumilia kusubiri Tume ya Uchaguzi kukamilisha shughuli yake.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari, kiongozi wa Ujumbe wa waangalizi hao kutoka Umoja wa Ulaya Alojz Peterle amesema, “Cha muhimu zaidi wakati huu ni kuendelea kudumisha amani. Huu ni wakati ambao ni mgumu hasa baada ya uchaguzi wowote ule. Wakenya wamedhihirisha kwamba ni wavumilivu lakini uvumilivu zaidi unahitajika katika kipindi hiki tulicho nacho sasa ambapo tunasubiri Tume ya IEBC kukamilisha kazi yake.”
Bwana Alojz amesema ujumbe wake utaendelea kuangalia kwa makini awamu zilizosalia kuhusiana na mchakato mzima wa uchaguzi na kwamba uwazi na kuaminika kwa uchaguzi mkuu unaweza kukadiriwa tu baada ya kujumlishwa kwa kura na kutangazwa kwa matokeo pamoja na kushughulikiwa kwa tetesi zozote zinazoweza kuzuka. Ujumbe huo wa Umoja wa Ulaya utaendelea kukaa nchini Kenya hadi tamati na kuwasilisha matokeo yake ya mwisho kwenye ripoti kamili miezi miwili ijayo.
Rais mpya kutangazwa Ijumaa
Shughuli ya kujumlisha kura inayoendelea katika ukumbi wa Bomas mjini Nairobi inatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa na mshindi wa urais kutangazwa. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, Issack Hassan anasema, "Ifikapo Ijumaa alfajiri tutaweza kuikamilisha shughuli hii. Hata hivyo endapo kutakuwa na matatizo yoyote yatakayosababisha kuchelewa kwa shughuli hii kumbuka kwamba tuna muda wa hadi Jumatatu kutangaza matokeo kwani hivyo ndivyo sheria inavyosema."
Kwa mujibu wa katiba, Tume ya Uchaguzi ina muda wa siku saba baada ya uchaguzi kukamilika kuweza kutangaza mshindi wa urais. Kukwama kwa shughuli ya uwasilishaji matokeo kwa njia ya elektroniki kulikuwa kumezua taharuki miongoni mwa Wakenya huku baadhi ya vyama vya kisiasa vikidai kwamba Tume ya Uchaguzi ilikuwa na njama ya kufanya udanganyifu kwa kura ya urais.
Ingawaje kurejelewa kwa shughuli hiyo kunafanyika polepole, kumerejesha imani ya wapigaji kura wagombea wanaosubiri matokeo pamoja na waangalizi wa uchaguzi huo. Uchaguzi huo ambao ni wa kihistoria chini ya katiba mpya umewafedhehesha vigogo wa kisiasa ambao wameshindwa kunyakua viti walivyokuwa wakiwania. Miongoni mwa wababe wa kisiasa walioangushwa ni pamoja na Mawaziri, Sam Ongeri, William Ole Ntimama, Amos Kimunya, Charity Ngilu na mwenyekiti wa chama cha ODM, Henry Kosgey.
Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Josephat Charo