Wade akabiliwa na changamoto kubwa Senegal
25 Machi 2012Abdoulaye Wade, ambaye kuwania kwake muhula wa tatu wa urais kumesababisha maandamano ya ghasia nchini Senegal, anakabiliana na changamoto kali kutoka kwa mshirika wake wa zamani Macky Sall katika uchaguzi huu wa duru ya pili.
Wade ameshindwa kupata wingi wa kutosha katika uchaguzi wa duru ya kwanza hapo Februari 26 mwaka huu akipata asilimia 34.8 tu ya kura. Sall alichukua nafasi ya pili akipata asilimia 26.6.
Wapinzani waungana
Wagombea wa duru ya kwanza wamejiunga pamoja na kumuunga mkono Sall kama ilivyo kwa kundi la vyama vya kijamii la M-23, ambalo limekuwa likitoa wito kwa Wade mwenye umri wa miaka 85, ajiuzulu.
Kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa duru ya pili haukuwa na matukio mabaya baada ya watu sita kuuwawa katika maandamano kabla ya duru ya kwanza.
Wade ana matumaini ya kurefusha kipindi chake cha miaka 12 madarakani kwa kuwashawishi wengi wa Wasenegali ambao hawakupiga kura katika uchaguzi wa hapo Februari na kuwachombeza viongozi wa kidini ambao wanaushawishi mkubwa katika nchi hiyo ambayo ina Waislamu wengi.
Umasikini umefutwa
Umasikini na idadi kubwa ya watu wasio na ajira vinabaki kuwa kero mbili kuu dhidi ya Wade, ambaye ameingia madarakani mwaka 2000. Anadai kuwa amefanya mambo mengi kuliko mahasimu wake wa Kisoshalisti walivyofanya katika muda wa miaka 40 ya kuwa madarakani tangu uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960.
Wade amesema wakati wa mkutano wake wa mwisho wa kampeni mjini Dakar siku ya Ijumaa, kuwa "umasikini umefutwa kutoka nchini Senegal, lakini sikatai kuwa kuna hali hiyo hapa na pale katika miji mikubwa. Nitalishughulikia suala hilo baada ya uchaguzi".
Kampeni zimejishughulisha zaidi na mzozo kuhusu haki ya kisheria ya Wade kuwania muhula wa tatu madarakani katika nchi hiyo ambayo inaonekana kuwa na demokrasia imara katika bara la Afrika. Juhudi yake ya kuwania tena madaraka iliidhinishwa na baraza la katiba, ambapo kiongozi wake amemteua yeye binafsi.
Wapiga kura wengi wanamuona Wade hivi sasa, ambaye alichaguliwa kwa wingi mkubwa mwaka 2000, kuwa ni mfano mwingine wa viongozi wa Afrika waliotawala kwa muda mrefu na wanaotaka kuendelea kung'angania madarakani.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri : Ndovie, Pendo Paul