1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wagoma nchini Afrika Kusini

13 Juni 2007

Mgomo mkubwa unaendelea nchini Afrika Kusini huku maelfu ya wafanyakazi wakijiunga na mgomo huo ambao umeingia katika siku ya kumi na mbili.

https://p.dw.com/p/CHkZ
Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini
Rais Thabo Mbeki wa Afrika KusiniPicha: AP

Shughuli mbali mbali zimekwama katika maeneo kadhaa nchini humo.

Huduma za usafiri katika baadhi ya miji nchini Afrika Kuisini, uzoaji takataka na hata shughuli za mahakama zimekwama kufuatia mgomo huo ulioitishwa na vyama vya wafanyakazi huku maandamano yakifanyika katika maeneo ya katikati ya miji 43 nchini humo.

Maelfu ya wafanyakazi wamejiunga na mgomo huo leo hii huku wafanyakazi wa serikali za mitaa wakijiunga na wenzao katika maandamno yaliayofanyika mchana leo mjini Johannesburg.

Polisi waliweka ulinzi mkali wakati wa maandamano hayo hakuna taarifa zozote za vurugu zilizoripotiwa wakati wafanyakzi hao walipoandamana kudai nyongeza ya mishahara.

Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Afrika Kusini COSATU umeapa kuilazimisha serikali kulishughulikia swala la nyongeza za mishahara.

Mwenyekiti wa muungano wa wafanyakazi bwana Willy Madisha ameonya kwamba mgomo huo ulioingia katika siku yake ya 12 utaendelea na utawahusisha takriban wanachama milioni mbili.

Mgomo huo unatishia kuzorotesha kabisa huduma za jamii na vile vile unatishia kuathiri uchumi wa nchi hiyo.

Licha ya rais Thabo Mbeki kudhani kuwa mzozo huo wa mishahara utatatuliwa kwa haraka, hadi sasa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa katika mazungumzo baina ya serikali na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kama anavyo eleza mwandishi mmoja wa habari kutoka Johannesburg

K. K. Nkosi, afisa wa cheo cha juu katika muungano wa wafanyakazi nchini Afrika Kusini COSATU anailaumu serikali kwa kuwapa mawaziri nyongeza ya asilimia 50 lakini wakati huohuo kuona vigumu kutoa nyongeza ya asilimia 10 kwa wafanyakazi.

Waziri wa kazi na mipango wa Afrika Kusini Geraldine Fraser Moleketi amewatolea mwito watu wanaogoma kurudi makazini ili kuwahudumia raia wa kawaida ambao wanateseka.