1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wa kiafrika walioko Israel waandamana

Sylvia Mwehozi
23 Februari 2018

Mamia ya wahamiaji wa kiafrika walioko kizuizini nchini Israel wameandamana siku ya alhamis pamoja na kuendelea na mgomo wa kutokula chakula wakipinga sera mpya ya Israel yenye utata ya kutaka kuwafukuza au kuwafunga. 

https://p.dw.com/p/2tCc3
Israel Migranten protestieren gegen israelische Asylpolitik
Picha: Imago/UPI Photo

Wahamiaji hao walitembea umbali mfupi kutoka kituo cha wazi cha Holot hadi gereza la Saharonim, wakipaza sauti na kutoa ishara za kutaka kuachiwa kwa wafungwa. Wanasema wamo katika mgomo wa kutokula chakula na wameapa kuendelea hadi ufumbuzi utakapopatikana .

Israel Flüchtlinge in Holot
Wahamiaji wa kiafrika katika kizuizi cha Holot Israel Picha: Getty Images/AFP/M. Kahana

Israel inajiandaa kuwarejesha maelfu ya wahamiaji wa Eritrea na Sudan walioingia nchini humo kinyume cha sheria na ambao maombi yao ya kuomba hifadhi hayako chini ya uchunguzi. Hata hivyo serikali imewapatia chaguo, kuondoka nchini humo hadi kufikia mapema mwezi Aprili au kukabiliwa na kifungo jela.

Wengi wanaweza kukabiliwa na hatari pindi watakaporejeshwa katika nchi zao, na hivyo Israel inapendekeza kuwapeleka katika nchi nyingine ya tatu isiyojulikana, ambapo wahamiaji na wafanyakazi wa misaada ya kiutu wanasema nchi hizo zinaweza kuwa ni Rwanda au Uganda.

Israel inapanga kwa kuanza kushughulikia kesi za wanaume ambao hawakuwasilisha maombi ya kuomba hifadhi, au ambao maombi yao yamekataliwa. Mamlaka nchini humo siku ya Alhamis ziliwahamisha wahamiaji wa Eritrea, waliokuwa kizuizini katika kituo cha wazi cha Holot na kuwapeleka jela ya Saharonim baada ya kukataa kuondoka nchini humo. Mamlaka hizo zilisema wahamiaji tisa ndio waliofungwa wakati wahamiaji wenyewe wakisema idadi yao ni 12.

Mamia ya wafungwa katika kituo cha wazi cha Holot walianza mgomo wa kutokula chakula kuanzia usiku wa Jumanne ili kupinga hatua hiyo. Na katika maandamano yao ya Alhamis, wahamiaji hao walipaza sauti wakisema "sisi sio wahalifu, ni wakimbizi, hakuna kurudishwa nyumbani! hakuna tena jela! Hatuko kwa ajili ya kuuzwa, sisi ni waomba hifadhi! Warejesheni kaka zetu".

Israel Asylsuchende
Waomba hifadhi kutoka Afrika wakiwa wameketi katika bomba la maji kwenye kizuizi cha HolotPicha: picture-alliance/Keystone/O. Weiken

Mhamiaji mmoja kutoka Eritrea Muluebrhan Ghebrihimet mwenye miaka 27, aliwasili nchini Isreal miaka sita iliyopita na ametuma maombi ya hifadhi lakini yalikataliwa. Anasema "tuko hapa kuomba hifadhi na sio kufanya kazi au kusaka utajiri". Kijana huyo hajui lini atapelekwa jela. Wimbi la wahamiaji wa kiafrika liliwasili nchini Israel mwaka 2007, wakivuka mpaka katika rasi ya Sinai nchini Misri. Njia hiyo isiyo salama ilidhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kukomesha wahamiaji kuingia nchini humo.

Wahamiaji hao waliishi katika vitongoji maskini kusini mwa Tel Aviv, mji mkuu wa kibishara lakini uwepo wao umesababisha msuguano na Waisrael wengine. Viongozi wa kidini na wahafidhina, akiwemo waziri mkuu Benjamin Netanyahu wamesema kuwa Waislamu na wahamiaji wa kikristo ni kitisho kwa utambulisho wa kiyahudi.

Serikali inayohesabiwa kuwa ya mrengo wa kulia katika historia ya Israel, imeshutumiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, wasomi na makundi ya haki za binadamu kuhusu mpango wake kuhusu wahamiaji. Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya mambo ya ndani, Israel ina wahamiaji karibu 42,000 wa Kiafrika, nusu yao ni watoto, wanawake au wanaume na familia zao ambao hawakabiliwi na mpango huo wa mwezi Aprili wa kurejeshwa nyumbani. Maafisa wa Israel wanasisitiza kwamba yeyote wanayemuhesabu kama mkimbizi au muomba hifadhi hatorejeshwa nyumbani.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Saumu Yusuf