Wahanga wa mafuriko waazimia kufunga Ramadhan
11 Agosti 2010Licha ya maafa hayo yote,wahanga wa mafuriko wanasema,maafa sio sababu ya kutofunga mwezi huu mtukufu wa Ramadhan. Nchini Pakistan,mwezi wa Ramadhan unaanza kesho Alkhamisi, kinyume na nchi nyingi zingine za Kiislamu ambako leo ndio siku ya kwanza ya mwezi wa Ramadhan. Wahanga wa mafuriko ya Pakistan, waliopoteza nyumba, vyakula, mifugo na mazao yao ya mashambani, hawana mahala pa kuishi na wanategemea msaada wa chakula. Lakini licha ya dhiki hizo zote, wengi wao wanasema kuwa watafunga kama kawaida mwezi huu wa Ramadhani, hata ikiwa hawajui futari yao itatoka wapi au kama itapatikana. Mungu ndie anayejua.
Pakistan ina watu milioni 165 na wengi wao ni Waislamu, na licha ya kujulikana kuwa inatumiwa na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu kama mahala pa maficho, Waislamu wengi wa Pakistan wana msimamo wa wastani ambao ni wahafidhina wenye kufuata kwa dhati imani za dini yao. Juhudi kubwa za kimataifa kupeleka misaada nchini humo zinapamba moto ili kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo. Baadhi ya wafanya kazi wa misaada, wanahofia kwamba Ramadhan inaweza kuhatarisha afya za watu ambao tayari wanakabiliwa na uhaba wa chakula, na hiyo kuzifanya juhudi za kufikisha misaada kuwa ngumu zaidi.
Daktari mmoja anayeshughulikia misaada amesema, watu wanaopata lishe duni, hawako katika hali nzuri ya kufunga, ingawa kujiepeusha na kula na kunywa kwa kutwa nzima, kunaweza kuwalinda watu dhidi ya magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya maji machafu. Akifafanuwa zaidi, Dr.Ahmad Shadoul amesema, kwa hakika watu hao hawako katika hali nzuri ya kuweza kufunga, kwa vile chakula wanachokula sio cha kutosha.
Kwa upande mwengine, amesema funga inaweza kuwa hatua ya kinga kwa magonjwa ya kuharisha, kwani watu hawanywi maji kwa masaa 14 hadi 15. Masaa ya kazi katika nchi nyingi za Kiislamu hupunguzwa wakati wa mwezi wa Ramadhan ambapo mara nyingi watu hupungukiwa na nguvu.Ingawa wahanga wengi wa mafuriko hayo wanakabiliwa na njaa na wengine hata na magonjwa, hali hiyo haikuwayumbisha na imani yao.
Mwandishi:P.Martin/RTRE
Mhariri: Othman,Miraji