1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa kimataifa wakutana kujadili Mazingira Stolkholm

2 Juni 2022

Baada ya miaka 50 ya Sweden kuwa mwenyeji wa kwanza wa mkutano wa kihistoria wa kimataifa kuhusu mazingira,wajumbe warudi tena Stolkholm kutafuta njia za kutekeleza mikataba iliyofikiwa.

https://p.dw.com/p/4CD25
Schweden Stockholm | Antonio Guterres und Magdalena Andersson
Picha: JONATHAN NACKSTRAND/AFP/Getty Images

Mkutano wa kimataifa wa mazingira umefunguliwa leo mjini Stolkholm Sweden ikiwa ni baada ya miaka 50 ya mkutano wa kwanza kabisa wa mazingira wa Umoja wa Mataifa kufanyika nchini humo. Agenda ya mkutano huo ni kutazama namna ya kuharakisha mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani. 

Picture gallery - the world’s most important forests
Picha: McPHOTO/G. Streu/picture alliance

Wajumbe chungunzima wakiwemo mawaziri, viongozi kadhaa wa serikali na wanaharakati wanashiriki mkutano huo wa kimataifa wa siku mbili. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutterres pia ni miongoni mwa wanaoshiriki.

Katika ufunguzi wa mkutano huo mfalme Gustaf wa Sweden aliwahutubia wajumbe waliofika kutoka nchi mbali mbali za ulimwengu akitazama nyuma kwenye mkutano wa kwanza wa  kihistoria wa mazingira uliowahi kufanyika katika nchi hiyo miaka 50 iliyopita mnamo mwaka 1972.

Mfalme huyo amekumbusha kwamba wametoka mbali tangu wakati huo lakini kilicho wazi ambacho amekisisitiza ni kwamba ulimwengu hauna miaka 50 mengine ya kubadilisha hali inayoshuhudiwa. Ametahadharisha kuhusu mgogoro wa kimazingira kwa kuongeza kusema kwamba ikiwa ulimwengu unataka kuzuia ongezeko la joto duniani miaka michache ijayo ni kipindi muhimu sana kufanikisha hilo.

Royals | Schweden | Königspaar Carl XVI. Gustaf und Silvia
Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kwa upande mwingine waziri mkuu wa Sweden Magdalena Andersson nae amekumbusha kwamba mapambano ya kukabiliana na mgogoro wa mazingira sio jukumu la nchi moja.

"Kilichofanyika miaka 50 iliyopita hapa Stolkholm ni kwamba tuliyaweka masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabia nchi katika agenda za masuala ya siasa ya kimataifa. Tukitambua kwamba pia hiki sio kitu- kitakachofanikishwa na nchi moja au nchi chache, lakini tunapaswa kukifanikisha kwa pamoja''

Mkutano huo unaosimama na kauli mbiu inayosema dunia salama kwa ajili ya maendeleo ya watu wote- "jukumu letu, fursa yetu'' utajikita katika kutazama njia za kuimarisha utekelezwaji wa makubaliano yaliyopo kuhusu mazingira kama vile makubaliano ya Umoja wa Mataifa ya malengo ya maendeleo endelevu pamoja na ule uliofikiwa mjini Paris kama ambavyo pia amefafanua waziri mkuu wa Sweden-Andersson.

''Na kwa hivyo lengo la mkutano wa leo ni kwamba kila mmoja atarudi nyumbani na kuhakikisha anachukua hatua zaidi na za haraka''

Achim Steiner Direktor UN-Umweltprogramm UNEP
Picha: AP

Hakutarajiwi kufikiwa makubaliano mengine mapya wala maamuzi mengine katika mkutano huo wa Stolkholm.

Stockholm ndiko ulikofanyika mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira mnamo mwaka 1972 na pia kikao hicho ndicho kilichoasisi shirika la mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa UNEP.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW