Matibabu bado ni changamoto Kenya licha ya mashine za kisasa
17 Februari 2020
Benki ya Dunia iliisifu Kenya baada kutangaza kuanzisha mpango wa afya wa kukodisha mashine za kisasa kutoka kwa makampuni makubwa ya kigeni. Katika makubaliano na serikali ya Kenya, makampuni hayo yalipewa kandarasi za kuweka na kutengeneza mashine hizo katika hospitali za Kenya.
Katika mpango huo ulioanza mwaka 2015, Kenya inakadiriwa kuwa ilitumia takriban dola milioni 370 kununua mashine hizo kutoka kwa makampuni ya Phillips, General Electric, kampuni ya China ya Shenzhen Mindray na Esteem Industries kutoka India.
Katika mpango huo wa miaka saba ambao ulisisfiwa na wakopeshaji wa kimataifa kama mpango mkubwa zaidi wa afya barani Afika, serikali hiyo ilibidi kuyalipa makampuni ya kigeni mamilioni ya pesa kununua na kukodisha mashine za kisasa za afya.
Lakini mbunge Mutula Kilonzo, ambaye yuko kwenye kamati iliyochunguza makubaliano kati ya serikali ya Kenya na makampuni hayo, anasema huenda pesa mara mbili zilitumiwa kwani wizara ya afya iliagiza mashine nyingine.
Je Wakenya wamenufaika na mpango huo?
Kufikia sasa, Benki ya Dunia bado inayashawishi mataifa mengine ya Afrika kufuata mkondo wa Kenya, kwani mpango wa kukodisha na kununua mashine za kisasa kwa makampuni huhakikisha kwamba mashine za hospitali zinatengenezwa vizuri, kulingana na benki hiyo.
Mtaalamu mkuu wa masuala ya afya wa benki hiyo barani Afrika, Khama Rogo, amesema kuwa ijapokuwa Kenya haijafanikiwa vizuri katika kutekeleza mpango huo, bado mpango huo ni mzuri kwa mataifa mengi Afrika. Aidha amesema kuwa Kenya haikufuata ushauri wa benki hiyo katika kufanya mpango huo.
Mnamo mwaka 2015, Kenya ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kutekeleza mpango huo ambao unatumiwa katika mataifa yalioendelea.
Lakini miaka mitano tangu mashine hizo kuchukuliwa katika hospitali kadhaa nchini humo, bado hazitumiwi, kwa mujiibu wa wizara ya afya na muungano wa madaktari. Muungano wa madaktari unasema ukosekanaji wa umeme na vifaa vya msingi kama vile glovu unawalazimisha kutumia njia mbadala kama vile mwangaza wa simu za mkononi katika kufanya upasuaji katika hospitali kadhaa.
Katika hospitali la King Fahad katika Kaunti ya Lamu, afisa mkuu wa afya kaunti hiyo, Ann Gathoni, alisema mashine ya CT-Scan iliyotolewa kwa hospitali hiyo haifanyi kazi kwa kukosa ya kuiwezesha kusoma picha za mionzi. Wagonjwa husafiri hadi Mombasa ili kuwezea kupigwa picha ya kichwa.
''Inasikitisha kwamba serikali iishindwa kuboresha afya, ikaamua kufanya ununuzi wa mashine hizo," alisema Daktari Ouma Oluga, mkuu wa Mungano wa Madaktari nchini Kenya, ambaye anauita mpango huo kuwa ni 'uhalifu.'
Katika hospitali kuu za Naivasha na Embu, wagonjwa wengi wamesaidiwa na mashine za kusafisha damu kwa figo, madaktari katika hospitali hizo wameliambia shririka la habari la Reuters.
Watu wengi huhitaji tu huduma msingi za afya, lakini mashine dhana zinakuwezesha kupata kura nyingi hata kama hazitumiwi, anasema Daktari Githinji Gitahi, Mkrugenzi Mkuu wa Amref Health Africa.
Lakini baada ya miezi tisa tangu tangazo hilo kutolewa, wagonjwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu wa takribani kilomita 160 kutoka maeneo ya katikati mwa Nyandarua hadi Hospitali Kuu ya Kenyatta, ambapo pia huchukua miezi kadha kabla ya kupigwa picha kwa mionzi, kwani katika eneo hilola Nyandarua hakuna daktari wa huduma hiyo.
Usaliti dhidi ya uaminifu
Makampuni ya General Electric, Medtronic na Philips yaliwaambia wanahabari kuwa yalitimiza makubaliano yake na Kenya katika kandarasi kwa kuweka mashine katika hosptali. General Electric imesema ilichukua mashine zipatao 585 kwa moja ya makubaliano, lakini mikaeleza kuwa 13 kati ya mashine hizo bado zinatengenezwa ili kuweza kufanya kazi.
Aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Edwad Ouko, ameeleza kwamba serikali ya nchi hiyo haikufanya utafiti kuhusu mahitaji ya hospitali nyingi kabla ya kuanza kusambaza mashine na vifaa kadhaa kutoka kwa makampuni ya kigeni.
Mara kadhaa, serikali ilikata kusikiliza pendekezo lake la kutaka kuhakiki mikataba kati ya serikali na makampuni ya kigeni kuhusu makubaliano ya kununua vifaa na mashine za kisasa za matibabu, ''makubaliano hayo ulikuwa ni usaliti kwa uaminifu wa mlipaji ushuru'', anasema mwanasheria huyo.
Wakosoaji wa mpango huo wanasema uliongeza deni kwa taifa la Kenya, na kuilaumu serikali kwa kutumia vibaya pesa ambayo ingeweza kutumiwa kwa kuboresha afya kwa Wakenya wengi.
Mnamo Oktoba, Waziri wa Afya Sicily Kariuki aliliambia bunge kuwa serikali ilisaka ushauri kuhusu mpango huo kutoka kwa viongonzi wa kaunti mbali mbali, jambo ambalo magavana watano wamekanusha.
Chanzo: RTRE