Wakenya watakiwa kuwacha kuwanyanyasa wagonjwa wa COVID 19
23 Aprili 2020Kwenye hotuba kwa vyombo vya habari, Wizara ya Afya imesema kuwa visa hivyo vimetokana na hatua ya kuwapima watu 668 ambapo visa saba viliripotiwa kupatikana Mombasa na vingine vitano vikapatikana Nairobi, huku wagonjwa hao wakiwa na kati ya umri wa miaka 22 hadi 60. Habari njema ni kuwa watu sita waliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata nafuu.
Daktari Mercy Mwangangi amewaambia Wakenya kuwa Wizara ya Afya ingali inachunguza athari za mikakati iliyowekwa na serikali ambayo itatolewa hivi karibuni. Mikakati hiyo itaelezea iwapo vituo vya karantini vitafungwa ama vitataendelea kuwepo, baada ya hisia kali kutolewa na wakenya wanaosema kuwa vituo hivyo vinakiuka haki za binadamu.
''Kuambukizwa virusi vya corona sio makosa, sote tuko kwenye hatari ya kuambukizwa. Kuwekwa kwenye karantini sio kifungo ama adhabu, ni kwa maslahi mapana,” alisema daktari Mercy Mwangangi
Watu wawili kati ya 50 waliotoroka kwenye kituo kimoja cha karantini mapema juma hili jijini Nairobi wamekamatwa huku wengine 48 wakiendelea kutafutwa. Pindi watu hao watakapokamilisha muda wao katika kituo cha karantini watashtakiwa kwa makosa ya uhalifu.
Rais wa Kenya asema mikakati ya kukabiliana na Corona haitalegezwa
Huku mwezi mtukufu wa Ramadhan unapokaribia, rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa mikakati iliyowekwa na serikali yake ya kukabiliana na janga la covid-19, haiwezi kulegezwa ili kuwaruhusu waumini wa dini hiyo kutekeleza.
Wakati huo huo Waziri wa Fedha Ukur Yattani ametakiwa kufika mbele ya Seneti kuelezea matumizi ya dola milioni nne sawa na shilingi bilioni 40 za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya. Hatua hiyo inajiri baada ya wakenya kuelezea hisia kali kuwa serikali haikuwapa uzito ilipokuwa inatengea fedha hizo sekta mbali mbali.
Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa fedha hizo zinastahili kutumika kwenye sekta ya afya na teknolojia ili kuwanufaisha wananchi bila ya kuwepo kwa urasimu pindi zinapohitajika.
"Sitaki kusikia visingizio visivyo na msingi vya kucheleweshwa kwa fedha hizo ama kutatizwa kwa mikakati iliyowekwa na sekta ya kibanafsi na wafanyikazi wa umma,”alisema rais Uhuru Kenyatta.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari hii leo, mwenyekiti wa kamati ndogo ya seneti inayokabiliana na janga la Covid 19 Johnson Sakaja ameagiza waziri Yattani kufanya hivyo kwa kipindi cha saa 24 zijazo.
Sakaja ameongeza kusema kwenye taarifa yake kuwa, iwapo waziri huyo hatafika mbele ya kamati yake atatumiwa nyaraka za kisheria za kumlazimisha kufanya hivyo. Yattani hakufika mbele ya kamati hiyo mapema leo asubuhi kwa kuwa alikuwa na mkutano na rais katika ikulu, wamesema, wasaidizi wake.
Chanzo: Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi