Wakimbizi wanakabiliwa na hatari ya kukosa makaazi
23 Mei 2016Ukizindua kampuni ya dunia inayojulikana kama " hakuna mtu atakayeachwa nje", shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi limesema bado linahitaji dola nusu bilioni kuwapatia wakimbizi makaazi.
"Bila ya kuwa na ongezeko kubwa la fedha na msaada wa dunia, mamilioni ya watu wanaokimbia vita na kukamatwa wanakabiliwa na hali ya kutokuwa na makaazi ama ukosefu wa nyumba katika nchi kama Lebanon, Mexico na Tanzania," shirika la UNHCR limesema katika taarifa.
"Bila kuwa na makaazi salama kula , kulala, kusoma,kuhifadhi mali zao na kuwa na faragha, kitakachotokea kwa afya zao na kijamii kinaweza kuwa kibaya zaidi," shirika hilo limeonya.
Mizozo, ikiwa ni pamoja na vita vya miaka mitano nchini Syria , vimechochea mzozo duniani ambapo watu wapatao milioni 60 wamekimbia makaazi yao duniani kote.
Sekta ya binafsi
Karibu watu milioni 20 kati yao wamelazimika kukimbia katika nchi mbali mbali dunia kama wakimbizi.
Kampeni ya UNHCR ina lenga kupata kupata fedha kutoka sekta ya binafasi kujenga ama kuimarisha makaazi kwa karibu wakimbili milioni mbili ifikapo mwaka 2018Shirika hilo linanununua mahema 70,000 kila mwaka na zaidi ya maturubai milioni mbili , na nje ya makambi shirika hilo linasaidia wakimbizi kupata nyumba na kulipia kodi.
Interpol na Europol
Wakati huo huo shirika la polisi la kimataifa Interpol na shirika la polisi la bara la Ulaya Europol jana yameonya kuhusu kuongezeka kwa wasi wasi kwamba Waislamu wenye itikadi kali huenda wakatumia mifumo haramu ya kuwasafirisha watu kupenya na kuingia katika bara la Ulaya ama hata kugharamia mashambulizi yao na shughuli zao.
Katika ripoti ya pamoja iliyowasilishwa jana, mashirika hayo mawili ya polisi yamesema wale wanaowatumia wakimbizi wamejikingia dola bilioni 6 mwaka jana. Hali hiyo imeweza kufanya mmiminiko wa wakimbizi kuwa moja kati ya vitu vinavyoingiza fedha nyingi zaidi kwa ajili ya uhalifu wa kupangilia katika bara la Ulaya.
"Magaidi wanaweza kutumia fedha za kuwaingiza wahamiaji kimagendo kutimiza malengo yao," imesema ripoti hiyo iliyotolewa na shirika hilo la polisi duniani mjini Lyon na Europol mjini The Hague.
Na mjini Rome kunafanyika mkutano wa ngazi ya mawaziri kutoka barani Afrika na Italia unaohudhuriwa na mawaziri kutoka nchi 40 za Afrika kujadili uhamiaji, usalama na masuala ya kiuchumi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman