1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanahabari wakandamizwa DRC

Admin.WagnerD24 Mei 2013

Shirika la wanahabari wasiokuwa na mipaka limeripoti kuwa maisha ya waandishi wa habari Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo yamo hatarini na wanazuiliwa kuripoti kwa uhuru maeneo yanayodhibitiwa na kundi la waasi la M23

https://p.dw.com/p/18dWA
Picha: AP

Katika taarifa waliyoitoa hapo jana, shirika hilo la kimataifa limesema baada ya kuwahoji waandishi wa habari katika jimbo la Kivu ya kaskazini limebaini kuwa vyombo vya habari vinatishwa,kuchunguzwa hasa kuhusiana na sera zao za uhariri na hata wakati mwingine kutekwa nyara kwa wafanyakazi wa mashirika hayo ya habari na waasi wa kundi la M23.

Shirika hilo la RSF limesema kuwa taaluma ya uandishi habari katika eneo hilo la mashariki mwa Congo imo katika hatari ya kutokomea. Mhariri mmoja katika eneo hilo ameliambia shirika hilo kuwa maafisa wa kijasusi wa kundi hilo la M23 huja kila jioni katika afisi zao na kupitia ripoti zao zote na ndio wanaoamua ni gani zinapaswa kupeperushwa hewani kwa ajili ya wasikilizaji na zipi wazitupilie mbali.

Ramani ya Kivu
Ramani ya Kivu

Mhariri huyo ameongeza kuwa kamwe hawawezi kukataa kutimiza matakwa ya waasi hao kwani kwa kufanya hivyo,ni kuhatarisha maisha yao.Inaripotiwa kuwa zaidi ya waandishi habari 10 wametoroka eneo hilo kwa kuhofia ukandamizaji na maisha yao.

Vyombo vya habari vyatatizika

Baadhi ya vituo vya redio vimesitisha matangazo yao na vingine vimelazimika kufunga.Ni kituo kinachofadhiliwa na Umoja wa Mataifa caha Redio Okapi pekee kilicho na makao yake katika mji mkuu Kinshasa ambacho kinaendesha shughuli zake bila muingilio wala matatizo yoyote kutoka kwa waasi hao.

Na sio waasi pekee wanaowahangaisha wanahabari katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, kulingana na shirika la RSF; serikali pia inafuatilia nyendo zao kwani inawashuku kwa kuwaunga mkono waasi wa M23. RSF inanukuu kisa kimoja ambacho meneja wa kituo kimoja cha redio amekuwa akizuiliwa kwa wiki tano sasa mjini Goma kwa madai ya kushukiwa kupeleleza shughuli za serikali kwa ajili ya M23.

Eneo la mashariki mwa Congo lina utajiri mkubwa wa madini na limekuwa likikumbwa na vita kwa zaidi ya miongo miwili na hali bado ni ya msukosuko hadi leo.Baada ya utulivu tete wa miezi adhaa,mapigano yalizuka upya tangu Jumatatu wiki hii kwa siku tatu mfululizo kati ya majeshi ya serikali na waasi hao.

Ban ki Moon akiwa Goma
Ban ki Moon akiwa GomaPicha: Reuters

Mapigano hayo yalisababisha vifo vya watu watatu na wengine takriban 10 kujeruhiwa na kusababisha maelfu kukimbilia usalama wao siku chache kabla ya ziara ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon siku ya Alhamisi wiki hii.

Shirika la waandishi habari wasio na mipaka RSF limesema lina wasiwasi kuhusu usalama wa wanahabari kutokana na hali mbaya ya usalama hasa suala la kuzuiwa kuripoti kwa uhuru,madai ambayo waasi wameyakanusha.

Mkuu wa masuala ya mawasiliano wa M23 Rene Abandi amesema ripoti hiyo ya RSF ni uongo mkubwa na kwamba M23 ni waathiriwa wa ushahidi wa uongo na kuongeza kuwa serikali ndiyo inahusika katika kupaka tope sifa ya kundi hilo.

Abandi amesema ana hakika kuwa kundi lao linataka uhuru kwa vyombo vya habari na linataka wakereketwa wao waweze kujielezea na kuongeza kuwa kiongozi wa kundi hilo Bertrand Bisimwa yeye mwenyewe alikuwa mwandishi habari.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon wakati wa ziara yake katika nchi hiyo siku ya Alhamisi ameahidi kuharakisha kutumwa kwa kikosi cha jeshi la Umoja huo ili kukabiliana na waasi hao na kusema wanajeshi hao watarajiwe nchini humo katika kipindi cha mwezi mmoja au miwili ijayo.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Mohammed Khelef