Wanajeshi wa upinzani Sudan Kusini waliwateka wanawake: UN
19 Oktoba 2018Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imesema wanajeshi wa upinzani nchini Sudan Kusini waliwateka wanawake na wasichana walio na umri wa hadi miaka 12 na kuwapanga msitari ili makamanda wa jeshi hilo waweze kuchagua wake na wale ambao hawakuchaguliwa walibakwa mara kadhaa na wanamgambo wengine.
Ripoti hiyo, iliyozingatia ushahidi wa wahanga na mashuhuda inaibua maelezo mapya kuhusiana na kuongezeka kwa vitendo vya machafuko na unyanyasaji vinavyoendelea kutokea hata baada ya makundi yanayohasimiana kufikia makubaliano hivi karibuni, juu ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano.
Mkuu wa haki za binaadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Brachelet amesema kwenye taarifa yake kwamba raia wengi waliotekwa bado wanashikiliwa.
Ripoti hiyo inaangazia eneo la Ikweta ya Magharibi, kati ya mwezi Aprili na Agosti, ikisema watu 900 walitekwa na wengine 24,000 walilazimishwa kuyakimbia makazi yao kutokana na kuongezeka kwa mapigano.