1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi walaumiwa kuuwa watu 34 nchini Kongo

22 Desemba 2016

Shirika la haki za binadamu limesema watu 34 waliuwawa na walinda usalama nchini Kongo katika maandamano ya kumpinga Rais Kabila anayeendelea kubakia madarakani baada ya muhula wake kumalizika rasmi tarehe 20 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/2UjSb
DR Kongo Unruhe vor Präsidentschaftsende von Joseph Kabila
Picha: Reuters/T. Mukoya

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu kanda ya Afrika ya Kati Ida Sawyer amesema kwamba watu wotw hao waliuwawa siku ya jumanne kwenye maandamano hayo hatua ambayo imeongeza idadi ya vifo kutokea watu 26 hadi watu 34.  Serikali ya Kongo hata hivyo imesema kuwa idadi ya watu waliokufa ni 22 akiwemo afisa mmoja wa polisi.

Mazungumzo ya kutafuta njia za kutatua mzozo wa kisiasa yanayoendeshwa na kanisa katoliki yanatarajiwa kuendelea.Wakati huo huo jeshi la Kongo limezingira eneo la Matshipisha-Gbadolite katika mji wa Lubumbashi kutokea mwendo wa saa 11 alfajiri na limefanya operesheni kubwa ya kuwakamata watu. Polisi wametoa taarifa kwamba watu 22 waliuwawa mjini Kinshasa, Lubumbashi mji ulio kusini mashariki, Matadi pamoja na mji ulioko magharibi wa Boma. taarifa ya polisi imeeleza kuwa watu wengine wanane waliuwawa katika eneo la Matshipisha na watu wengine 47 wamejeruhiwa. Idadi hiyo hata hivyo inapingwa na shirika la kutetea haki za binadamu.  Shirika hilo linasema kwamba jumla ya 34 wameuwawa.

Kwa mujibu wa watu ambao wameshuhudia operesheni hiyo, wamesema kuwa wanajeshi wanawakamata wanaume vijana kwa wazee wasio na vitambulisho na hata wale walionavyo. Haut-Katanga eneo kuu la mji wa Lubumbashi ni sehemu iliyo na wafuasi wengi wa mmoja wa viongozi wa upinzani Moise Katumbi.  Chama kikuu cha upinzani chini ya mwenyekiti wake Etienne Tshisekedi mwenye umri wa miaka 84 amewatolea mwito raia wa Kongo kuendeleza mapambano yanayozingatia amani.

Kongos Tschisekedi ist nach Kinshasa zurückgekehrt
Etienne Tshisekedi kiongozi wa upinzani nchini DRC Picha: picture-alliance/AP Photo/P Photo/J. Bompengo

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haijawahi kushuhudia utulivu na amani katika kubadilishana wa madaraka tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wabelgiji mnamo mwaka 1960. Rais Joseph kabila amekuwa madarakani tangu baake Laurent kabila alipouwawa kwa kupigwa risasi mwaka 2001. Rais Kabila alichaguliwa mnamo mwaka 2006 na kufikia mwaka 2011 alichaguliwa tena.  Katika miongo miwili iliyopita jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetumbukia kwenye vita vibaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya leo.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef