Mashambulizi ya Israel yaua Wapalestina 18 Gaza
15 Desemba 2024Msemaji wa shirika hilo, Mahmud Bassal, aliiambia AFP kuwa waokoaji waliokuwa wakifanya kazi usiku kucha walipata miili ya watu 18. Alisema makumi ya wengine walijeruhiwa katika "mashambulizi yanayoendelea ya anga na mizinga ya Israeli" kote Gaza.
Waliouawa ni pamoja na watoto wasiopungua watatu, alisema Bassal, na kuongeza kuwa watu wanne waliuawa katika shambulio la anga la Israeli lililolenga nyumba moja katikati mwa Jiji la Gaza.
Wengine wanne waliuawa, na wanane kujeruhiwa, wakati kombora la Israeli lilipolenga hema lililokuwa na makazi ya watu waliokimbia makwao huko Deir el-Balah, katikati mwa Gaza.
Picha za AFP zilionyesha hali ya huzuni wakati jamaa walipochukua miili ya wapendwa wao kutoka hospitali ya mji wa Gaza, huku miili mingine ikiwa imelazwa sakafuni ikiwa imefunikwa na blanketi.
Jumamosi, Bassal alisema kuwa meya wa Deir el-Balah, Diab al-Jaro, aliuawa katika shambulio kama hilo.
Jeshi la Israeli baadaye lilidai kuhusika na shambulio hilo, likisema kuwa Jaro alikuwa "mpiganaji katika kitengo cha kijeshi cha Hamas."
Soma pia: Marekani yaona ishara ya makubaliano ya Gaza
Jumapili, jeshi la Israeli lilithibitisha kuwa lilifanya mashambulizi katika maeneo ya Beit Hanoun na Beit Lahia.
"Wanajeshi walishambulia magaidi kadhaa kutoka angani na ardhini, na magaidi wengine walikamatwa" huko Beit Hanoun, ilisema taarifa ya jeshi hilo.
"Mjini Beit Lahia, wanajeshi waliangamiza magaidi na kugundua na kuvunja idadi kubwa ya silaha, zikiwemo vilipuzi na maguruneti kadhaa," liliongeza. Taarifa hiyo haikueleza wakati oparesheni hizo zilipofanyika.
Kwingineko, jeshi liliripoti kushambulia kliniki kaskazini mwa Gaza, likisema Hamas iliitumia kama "kituo cha kamandi na udhibiti" na eneo la kuhifadhi silaha.
Vita hivyo vimesababisha idadi kubwa ya watu milioni 2.4 wa Gaza kuyahama makazi yao, huku wengi wakilazimika kukimbia mara kadhaa.
Mashambulizi ya Israeli yamekuwa yakiendelea kwa wiki kadhaa kaskazini mwa Gaza, yakidaiwa kuwa na lengo la kuzuia wapiganaji wa Hamas kujiimarisha tena.
Soma pia: Hamas yathibitisha kuanza kwa mazungumzo ya kusitisha vita Gaza
Kulingana na mashirika ya huduma za afya ya Gaza, uhaba mkubwa wa dawa na wafanyakazi wa matibabu vinaathiri vibaya mfumo wa afya, huku hospitali zikiendelea kushambuliwa.
Tangu Oktoba 7, 2023, takriban watu 1,208 waliuawa nchini Israeli, na zaidi ya 44,976 wameuawa Gaza, wengi wao wakiwa raia, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Chanzo: AFP