Wapiga kura wa Burma wateremka vituoni kuwachagua wabunge
7 Novemba 2010Wapiga kura milioni 30 wa Burma wameteremka vituoni hii leo kulichaguwa bunge na mabaraza ya mikoa.Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi kama huo kuruhusiwa na utawala wa kijeshi tangu zaidi ya miaka 20 iliyopita.Watawala wa kijeshi mjini Rangun wanawaruhusu wapiga kura katika nchi hiyo masikini ya Asia wayachague mabaraza mawili ya bunge na mabunge 14 ya mikoa.Hata hivyo wamejiwekea haki ya kuwateuwa robo moja ya wawakilishi wa taasisi hizo.
Mwanasiasa mashuhuri wa upande wa upinzani,mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel, bibi Aung San Suu Kyi anaetumikia kifungo cha nyumbani,ametoa mwito wa kususiwa uchaguzi huo.Chama chake,NLD kimepigwa marufuku.
Rais Barack Obama wa Marekani akiwa ziarani barani Asia amewataka viongozi wa kijeshi wa Burma wamuachie huru Aung San Suu Kyi.Waziri wake wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton amesema uchaguzi huo wa bunge unatoa sura halisi ya jinsi wanajeshi wanavyotumia vibaya madaraka.
Burma imekuwa ikitawaliwa na wanajeshi tangu mwaka 1962 na wameibadilisha jina ,na kuiita badala yake Myanmar.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,reuters,dpa
Mpitiaji:Mohamed Dahman