WASHINGTON : Korea Kaskazini yataka mazungumzo
2 Novemba 2006Wiki tatu baada ya kufanya jaribio lake la bomu la nuklea Korea Kaskazini imesema iko tayari kurudi tena kwenye mazungumzo ya pande sita kwa sababu serikali ya Marekani imekubali kujadili na nchi hiyo vikwazo vya kifedha dhidi yake jambo ambalo imesema lilipelekea nchi hiyo kususia mazungumzo hayo.
Akiwa katika Ikulu ya Marekani Rais George W. Bush amesema anataka mazungumzo juu ya mpango wa nuklea wa Korea Kaskazini yaanze haraka inavyowezekana na yafanikiwe.Bush amewaambia waandishi wa habari kwamba anatumai serikali ya Korea Kaskazini itakuwa imedhamiria kwa dhati haja yake ya kuzima mzozo huo wa hivi karibuni kabisa.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo wametahadharisha kwamba makubaliano hayo ya kuwa na mazungumzo mapya haimaanishi moja kwa moja kwamba taifa hilo la kikoministi limebadili nia yake.