WASHINGTON : Korea Kaskazini yatakiwa kufunga mtambo
15 Aprili 2007Marekani hapo jana imeitaka Korea Kaskazini kulialika mara moja shirika la nuklea la Umoja wa Mataifa kwenda nchini humo kuufunga mtambo wake wa nuklea wa Yongbyon wakati muda wa mwisho unaoitaka serikali ya nchi hiyo kuufunga mtambo huo ukiwa umepita.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeonya kwamba subira yake kwa Korea Kaskazini ina kikomo hata hivyo inaonekana kukubali ushauri wa China kuipa muda Korea kaskazini kutimiza wajibu wake chini ya makubaliano ya mataifa sita yaliofikiwa hapo mwezi wa Februari.
Jana ilikuwa ni siku ya mwisho kwa Korea Kaskazini kuanza kufunga mtambo wake huo wa nuklea wa Yongbyon lakini mjumbe mkuu wa masuala ya nuklea wa nchi hiyo amekaririwa akisema serikali yake inahitaji siku 30 zaidi kuufunga mtambo huo.