1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Marekani yaionya Korea ya kaskazini kutofanya jaribio la pili la kinyuklia

17 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD2B

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, bibi Condoleeza Rice, ameionya Korea ya kaskazini isifanye jaribio la pili la kuripua bomu la kinyuklia baada ya maafisa wa idara ya upelelezi ya Marekani kuthibitisha jaribio la kwanza la wiki iliopita kuwa lilikuwa la kinyuklia.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, bibi Condoleeza Rice, amesema vikwazo Umoja wa mataifa uliowekea Korea ya kaskazini ni tahadhari pia kwa Iran ikiwa itaendelea na mpango wake wa kinyuklia.

Bibi Rice anatarajia kuifanya ziara mwishoni mwa wiki hii katika nchi za Japan, Korea ya kusini na Uchina kwa lengo la kutafauta uungwaji mkono wa dhati wa azimio la Umoja wa mataifa la kuiwekea vikwazo Korea ya kaskazini.

Australia tayari imetangaza kuwa imepiga marufuku meli za Korea ya kaskazini kutia nanga kwenye bandari zake ikiwa ni katika mpango wa kutekeleza vikwazo vya kiuchumi na silaha dhidi ya Korea ya kaskazini.

Wakati Marekani ikionya kuhusu jaribio la pili, taarifa ambazo Japan inazifanyia uchunguzi, zinasema huenda Korea ya kaskazini inajiandaa kwa jaribio la pili la kuripua bomu la kinyuklia.