WASHINGTON: Rais Bush asema jaribio la Korea Kaskazini linahatarisha usalama na amani duniani
9 Oktoba 2006Rais George W Bush wa Marekani amesema jaribio la nyuklia la Korea Kaskazini linahataraisha usalama na amani duniani. Amelaani vikali jaribio hilo akisema haliwezi kukubalika.
Amekubaliana na waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, kuchukua hatua kabambe dhidi ya Korea ya Kaskazini katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia jaribio la nyuklia.
Wakizungumza kwa njia ya simu viongozi hao pia wamekubaliana kuwa jaribio hilo ni tisho kubwa kwa usalama wa kimataifa na changamoto kwa juhudi za kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, ikiwa litathibitishwa rasmi.
Waziri mkuu Shinzo Abe alizungumza na rais Bush akiwa mjini Seoul alikokutana na rais wa Korea ya Kusini, Roh Moo-hyun.
Wakati huo huo, rais Bush na rais wa Urusi, Vladamir Putin, wamesisitiza umuhimu wa hatua ya pamoja dhidi ya Korea Kaskazini, lakini Urusi haijasema ikiwa itaunga mkono vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.