WASHINGTON: Rais George W.Bush aionya Korea ya kaskazini isizikabidhi silaha za kinyuklia Iran na Al-Qaida
19 Oktoba 2006Rais wa Marekani George W.Bush, ametoa onyo kali kwa Korea ya kaskazini kwamba itakabiliwa vikali ikiwa itajaribu kuikabidhi silaha za kinyuklia Iran au kundi la kigaidi la Al-Qaida la Ossama Bin Laden. Katika mahojiano na waandishi wa habari, rais Bush amesema atasimamisha shughuli hiyo ikiwa atapata ripoti juu ya hilo.
Wakati huo huo, waziri wake wa mambo ya kigeni, bibi Condoleeza Rice, ameihakikishia Japan kwamba Marekani itatumia uwezo wake wote kuilinda nchi hiyo dhidi ya kitisho cha kinyuklia cha Korea ya kaskazini. Bibi Rice aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tokyo, ikiwa ni katika hatua ya kwanza ya ziara yake katika nchi nne za eneo hilo. Kutoka Japan, bibi Rice ataelekea leo mjini Seoul Korea ya kusini, halafu Beijing-Uchina na hatimae Moscow nchini Rushia kutafuta mshikamano juu ya vikwazo vya Umoja wa mataifa dhidi ya Korea ya kaskazini kufuatia jaribio lake la kuripua bomu la kinyuklia wiki iliopita. Waziri wa mambo ya kigeni wa Rushia, Sergei Lavrov, kwa upande wake ameitolea mwito Korea ya kaskazini kuchukuwa hatua ya busara kuepusha mzozo mkubwa wa kinyuklia. Lakini wataalamu wa idara ya upelelezi wamesema vyombo vya ujasusi vya angani vilitambua gari ya kubebea zana za kijeshi ikishughulika katika kituo ambacho kinadhaniwa ni cha kufanyia majaribio ya kinyuklia na hivyo kuangazia juu ya uwezekano wa kufanyika jaribio la pili la kuripua bomu la kinyuklia.