WASHINGTON: Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani anaanza leo ziara katika nchi 4 jirani na Korea ya kaskazini
18 Oktoba 2006Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Condoleeza Rice, yuu njiani kuelekea Tokyo nchini Japan, ikiwa ni hatua ya kwanza ya ziara yake katika nchi 4 za eneo hilo. Lengo la ziara hiyo ni kutafuta uungwaji mkono wa dhati wa vikwazo Umoja wa mataifa ulioiwekea Korea ya kaskazini kufuatia jaribio lake la kuripua bomu la kinyuklia wiki iliopita.
Baada ya Japan, bibi Condoleeza Rice, atakwenda mjini Seoul-Korea ya kusini, Beijing-Uchina na Moscow nchini Rushia.
Bibi Rice atakabiliwa na kibarua kigumu kuihamasisha Uchina. Akiwahotubia wabunge, rais wa Uchina Hu Jintao, amesema kutekeleza vikwazo lazima kufanyike kukiwa kumehakikishwa kwamba hali itaendelea kudhibitiwa. Korea ya kaskazini ilisema mbinyu za Baraza la usalama la Umoja wa mataifa ni kama kuitangazia vita.