1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasi wasi juu ya hatima ya demokrasia na utawala wa vyombo vya kisheria Afrika kusini.

7 Aprili 2009

Ni baada ya Zuma kufutiwa mashtaka

https://p.dw.com/p/HS0j
Jaco Zuma katika moja wapo ya mikutano ya hadhara ya wafuasi wake.Picha: picture-alliance/dpa

Hatua ya kufutwa mashtaka yote ya rushwa dhidi ya Kiongozi wa chama tawala cha African National Congress-ANC nchini Afrika kusini Jacob Zuma, bila shaka imewafurahisha sana wafuasi wake, lakini wachambuzi wanaashiria kuwa haitoondoa kiwingu cha rushwa kinachotanda katika ngazi ya juu ya siasa za taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Kadhia hiyo imeitia dosari kwa kiwango fulani demokrasia ya 15 sasa, alau tangu ilipofichuka kashfa ya biashara ya silaha miaka 10 iliopita.

Swali linaloulizwa sasa ni ikiwa madai ya rushwa yataendelea kuikumba serikali ijayo chini ya uongozi wa Bw Zuma pindi akichaguliwa kama inavyodhaniwa na wengi, katika uchaguzi mkuu tarehe 22 mwezi huu na hivyo kushika wadhifa wa urais.

Mwendesha mashitaka mkuu wa Afrika kusini Mokotedi Mpshe alisema mapema juma hili kwamba miaka minane ya uchunguzi kuhusu udanganyifu, utumiaji mbaya na ulanguzi wa fedha dhidi ya Bw Zuma yanafutwa kwa sababu utaratibu mzima wa kisheria ulitumiwa vibaya na maafisa wa ngazi ya juu.

Hata hivyo mchambuzi wa masuala ya kisiasa Adam Habib kutoka taasisi ya utafiti wa kisayansi alisema hatua hiyo ina maana" utaratibu wa kisheria umetolewa mhanga lakini haimaanishi kuwa Zuma hana hatia na pamoja na hayo sura ya Afrika kusini kama jamii ya rushwa bado ipo pale pale."

Mwendesha mashitaka mkuu Mpshe aliyasoma mazungumzo yalionaswa katika kanda ambapo mtangulizi wake Bulelani Ngcuka na mkuu wa zamani wa kikosi cha kupambana na uhalifu " Scorpions" yaani nge Leonard McCarthy, walishirikiana kuandaa mshitaka dhidi ya Zuma kwa sababu za kisiasa.

Mazungumzo hayo yalionyesha kuna kinyanganyiro cha kuwania madaraka miongoni mwa vigogo ndani ya chama cha ANC. Uamuzi huo bila shaka ni afuweni kwa Zuma kwani kizingiti kimeondolewa na huenda hakuna chochote sasa cha kumzuwia asiwe rais . McCarthy sasa ni mkuu wa idara ya kupambana na rushwa katika Benki ya dunia.

Ni wazi kwamba wasi wasi uliopo ni Kuwa na rais anayekabiliwa na uwezekano wa kwenda jela ingekua ni dosari kubwa kwa sifa ya Afrika kusini nchi za nje ana sura ya Zuma binafsi nje na ndani ya nchi yake.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanasema ni bora wanaohusika na tuhuma za rushwa wakafikishwa mahakamani na kuiachia sheria ichukuwe mkondo wake badala ya swala hilo kuamuliwa na mwendesha mashitaka mkuu.

Wakosoaji wanasema ushindi wa Zuma unaweza kuzidisha hisia za kwamba imani mbele ya vyombo vya sheria inazidi kutoweka na Afrika kusini inakabiliwa na kitisho cha kujitoa katika maadili ya kidemokrasi iliokula kiapo kuyapigania na kuyalinda baada ya kumalizika utawala wa kibaguzi-Apartheid.

Alt Erzbischof Desmond Tutu, In My Name
Askofu mkuu Desmond Tutu.Picha: Roger Friedman

Hivi karibuni Askofu mkuu Desmond Tutu alikwenda umbali wa kutamka kuwa litakua ni kosa kubwa kwa chama cha ANC endapo Bw Zuma atafanikiwa kuwa rais wa Afrika kusini, matamshi ambayo yalisababisha wafuasi wa Zuma kumshambulia sana Askofu mkuu huyo na kuelezea masikitiko yao.

Kwa wafuasi wake Zuma chamani ,sasa watamtarajia awaondolee umasikini kama alivyoahidi ,kuwa atatumia fedha zaidi kwa ajili ya mamilioni ya walala hoi wa Afrika kusini, huku akiwaahidi wawekezaji kwamba hatoielekeza Afrika kusini katika siasa za mrengo wa shoto.

Mwandishi:M.Abdul-Rahman/AFPE