1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi iwapo Kenyatta atashinda uchaguzi

Hashimu Gulana 5 Machi 2013

Kuna wasiwasi kwamba ikiwa Uhuru Kenyatta atapata ushindi katika uchaguzi wa rais wa Machi 4 nchini Kenya, uhusiano wa kidiploamasia na kibiashara kati ya yake na nchi za Magharibi ukatetereka

https://p.dw.com/p/17lt1
Mgombea urais Kenya Uhuru Kenyatta
Mgombea urais Kenya Uhuru KenyattaPicha: picture-alliance/dpa

Uhuru Kenyatta anatuhumiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC kuhusika kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi Kenya wa mwaka 2007.

Wasiwasi huo umetolewa na wanadiplomasia wa balozi mbalimbali mjini Nairobi ambao wamesema kuwa, huenda mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia baina ya Kenya na mataifa hayo yakaingia dosari, iwapo Uhuru Kenyatta atashinda. Zaidi ya raia 1000 walipoteza maisha yao katika ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007/2008.

Taarifa hiyo imesema kuwa kushinda kwa Uhuru Kenyatta katika uchaguzi huo utayapa wakati mgumu madola makubwa na kuyaweka njia panda yakitafakari mustakhabali wa uhusiano baina yao na Kenya.

Uhuru Kenyatta na William Ruto
Uhuru Kenyatta na William RutoPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Mabalozi hao waliongeza kuwa iwapo Uhuru Kenyatta atashinda Urais wa nchi hiyo, kutaifanya Kenya kuwa nchi ya pili Afrika baada ya Sudan kuwa na kiongozi wa juu anayetuhumiwa na ICC kwa uvunjifu wa haki za binadamu.

Changamoto zinazomzunguka Uhuru Kenyatta

Uhuru Kenyatta ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya, hayati Jomo Kenyatta, anamkaribia mgombea wa Chama cha ODM ambaye pia ni Waziri mkuu wa nchi hiyo Raila Odinga katika kura ya maoni. Mgombea mwenza wake William Ruto pia anatuhumiwa na mahakama ya ICC kwa kuhusika katika ghasia za umwagaji damu wa 2007.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou BensoudaPicha: AFP/Getty Images

Wamesema kuwa kuna uwezekano wa kutorudi tena mahamani Uhuru Kenyatta baada kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo kama ilivyo sasa kwa Rais wa sasa wa Sudan Omar Hassan Al-bashir ambaye ametolewa hati mbili za mashataka dhidi ya haki za binadamu katika jimbo lenye machafuko la Darfur.

Kufuatia hali hiyo wanadiplomasia hao wamewataka wakenya kuona mfano hai wa Sudan ambayo inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa baada ya al-Bashir kugoma kufika kwenye mahakama ya ICC, ili kujibu mashitaka kuhusu mauaji ya halaiki jimboni Darfour. Wamesema kuwa Kenya nayo huenda ikakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi ambavyo vitakuwa na athari mbaya kwa raia wa nchi hiyo.

Mapema mwezi huu Rais wa Marekani Barack Obama alisema kuwa Marekani inaunga mkono na inakubaliana na utashi wa raia wa Kenya katika kumchagua rais wa nchi yao, ambapo pia mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa serikali ya Washington kwa ajili ya Afrika amedai huenda kukawa na athari kubwa kwa Kenya iwapo watuhumiwa hao wa ICC watashinda katika uchaguzi wa Machi 4, 2013.

Lakini huku hayo yakijiri, wanaomuunga mkono Uhuru Kenyatta wanayachukulia hayo madai na ICC kama sehemu ya mpango wa nchi za magharibi, kumuingiza Raila Odinga Ikulu, wakidai kuwa iwapo Mataifa ya magharibi yataicha Kenya baada ya ushindi wa Kenyatta, nchi hiyo itaimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi nyingine kama China.

Mwandishi: Hashim Gulana/ Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba