1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi Kenya kuhusu vituo visivyoweza kutuma matokeo

7 Agosti 2017

Wasiwasi umeibuka kuhusu tangazo la tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya IEBC, kwamba takriban asilimia 25 ya vituo vyake vya uchaguzi havina uwezo wa kutuma matokeo kwa mitandao

https://p.dw.com/p/2hoGv
Kenia Wahlen BOMAS Wahlkommission Archiv 2013
Picha: picture-alliance/dpa/F. Dlangamandla

Masaa machache kabla uchaguzi mkuu kufanyika nchini Kenya, wasiwasi umeibuka kuhusu hitilafu katika mipango ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo IEBC, baada ya kusema kwamba takriban asilimia 25 ya vituo vyake vya uchaguzi havina uwezo wa kutuma matokeo kwa mitandao licha ya kwamba wamekuwa wakiwahakikishia Wakenya kuwa mfumo huo wa kiteknolojia uko shwari. Aidha, mashirika ya kijamii katika Kaunti ya Baringo yanahofia kwamba baadhi ya wakaazi katika eneo hilo hawatoweza kushiriki zoezi la kupiga kura kwa kukosa vituo vya kupigia kura.

Changamoto za kiusalama

Chini ya masaa 24 kabla ya Wakenya hawajawachagua upya viongozi watakaowawakilisha serikalini, fikira ya kwamba baadhi yao hawatopata nafasi hii ni jambo linalowatatiza wakaazi wa Baringo wanaoiona hii kama fursa kwao kufanya uamuzi utakaowanufaisha.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akisikiliza mwandamanaji wa kundi la kijamii
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akisikiliza mwandamanaji wa kundi la kijamiiPicha: Reuters/B. Ratner

Mapema mwaka huu, machafuko baina ya jamii yaliyosababishwa na mashambulizi ya kisiasa pamoja na wizi wa mifugo katika maeneo ya Mukutani na Arabal, Kaunti ya Baringo, yalipelekea wakaazi kufurushwa makwao na kupewa hifadhi katika kambi 4 eneo la Eldume.

Hata hivyo, Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i anawahakikishia kwamba serikali itafanya mipango na tume ya IEBC kuhakikisha hata waliohamishwa kwa sababu ya machafuko watapiga kura.

Ukosefu wa vituo vya kupiga kura Baringo?

Hata hivyo, masaa machache kabla ya uchaguzi huo kufanyika, inaripotiwa kuwa baadhi ya maeneo ya Baringo hayana vituo vya kupigia kura, hasa eneo la Eldume, ambapo wakaazi kutoka Mukutani wanaishi katika kambi. Masese Kemunche ni mwakilishi wa mashirika ya kijamii yanayohudumu eneo la Baringo.

Gari la polisi kutumiwa katika kuimarisha usalama
Gari la polisi kutumiwa katika kuimarisha usalamaPicha: picture-alliance/Zuma/P. Siwei

Masese anakariri umuhimu wa tume ya IEBC kuzingatia hisia za Wakenya wakati huu ambapo kila mmoja ana mvuto wake wa kisiasa, na kwamba idara za serikali hazifai kuonekana kama zinaegemea upande mmoja. Aidha, kulingana naye, maafisa wa usalama hawajafanya vya kutosha kuwahakikishia Wakenya kwamba vikosi  vya kiusalama havitatumika kuchochea mapendeleo wakati wa uchaguzi.

Hii leo maafisa wa tume ya IEBC wako mbioni katika harakati za mwisho mwisho kuhakikisha kila pengo limezibwa tayari kwa uchaguzi mkuu hapo kesho. Tume hiyo imeeleza kuwa, katika maeneo ambapo vituo vya kupigia kura havitakuwa na uwezo wa mitandao, wasimamizi wa maeneo hayo watasongea hadi mahali watakapopata huduma hiyo. Vile vile tume hiyo itatoa mitambo ya satelaiti katika majimbo yote 290 nchini ili kuimarisha shughuli ya utumaji wa matokeo.
 

Mwandishi: Wakio Mbogho - DW, Nakuru

Mhariri: Mohammed Khelef