1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi watanda DRC wakati muda wa Kabila ukimalizika

19 Desemba 2016

Hali ya wasiwasi imetanda katika maeneo mengi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika siku ambayo muda wa Rais Joseph Kabila unafikia kikomo na mazungumzo ya kusaka suluhu kwa mkwamo wa kisiasa yakiahirishwa.

https://p.dw.com/p/2UWHX
Kongo Proteste gegen Joseph Kabila
Picha: Reuters/K. Katombe

Wafanyakazi na wanafunzi katika mji mkuu, Kinshasa, wanaripotiwa kuwa wamesalia majumbani mwao, huku idadi ya wanajeshi wanaofanya doria ikiwazidi watu wanaoonekana mitaani. 

Usafiri wa umma kwenye mji huo wenye shughuli nyingi pia umeathirika, ambapo abiria wachache wameonekana vituoni. 

Hata hivyo, mji huo wenye wakaazi wapatao milioni 10 uliripotiwa kuwa kwenye utulivu, ingawa maduka mengi yamefungwa katikati ya mji. 

Hali ya wasiwasi pia ilishuhudiwa kwenye maeneo mengine ya nchi, hasa Lubumbashi, Goma na Kisangani. 

Mwandishi wa DW aliripoti kumwagwa mitaani kwa wanajeshi na vikosi vyengine vya usalama katika miji ya Beni na Butembo, vinavyowazuwia raia kukusanyika zaidi ya watu wanne.

Meya wa mji wa Beni, Masumbuko Nyonyi, aliwataka raia kuendelea na shughuli zao kama kawaida, huku akionya dhidi ya maandamano. 

Muungano wa upinzani unaoongozwa na mkongwe Etiene Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 84, ulikuwa umetishia kufanya maandamano makubwa kuanzia leo Jumatatu (19 Disemba), ikiwa mazungumzo yangelifeli. 

Vipeperushi vinavyowataka watu "kuichukuwa Kinshasa, mtaa kwa mtaa, wilaya kwa wilaya, hadi tuichukuwe Kongo nzima" vimesambazwa kwenye mji mkuu huo.

Joseph Kabila Präsident Demokratische Republik Kongo
Muda wa Rais Joseph Kabila kikatiba unamalizika tarehe 20 Disemba 2016 lakini hakuna dalili ya kuachia madaraka.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Hata hivyo, hadi sasa upinzani umejizuwia kuwataka wananchi kuingia mitaani, huku jumuiya ya kimataifa ikitoa wito wa utulivu kwa pande zote. 

Mazungumzo ya kusaka muafaka

Muhula wa pili wa Rais Kabila unamalizia Jumanne (20 Disemba), lakini hajaonesha ishara yoyote ya kuondoka madarakani. Mazungumzo ya kusaka suluhu ya kisiasa yaliyokuwa yakiendeshwa na Kanisa Katoliki nchini humo yanaonekana kukwama, na sasa wasiwasi ni kwamba ghasia zinaweza kuzuka kwenye taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Kabila, mwenye umri wa miaka 45, anazuwia kikatiba kuwania muhula mwengine madarakani, lakini ameonesha kuwa anataka kubakia madarakani hadi pale mrithi wake atakapochaguliwa.

Hadi sasa, hakuna uchaguzi wowote uliopangwa na baadhi ya makundi ya upinzani yanamtaka kiongozi huyo kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito hadi hapo uchaguzi utakapoitishwa. 

Katika jaribio la mwisho la kusaka ukabidhianaji madaraka kwa njia za amani, mazungumzo yalifanyika kati ya chama tawala na baadhi ya makundi ya upinzani yanayojiambatanisha na muungano wa upinzani chini ya  Tshisekedi.

Lakini wiki moja baadaye, mazungumzo hayo yalivunjika siku ya Jumamosi, kukiwa hakuna hatua yoyote iliyopigwa kwenye masuala muhimu yanayozigawa pande hizo mbili. 

Kuna uwezekano wa mazungumzo hayo kuanza tena siku ya Jumatano (Disemba 21), siku moja baada ya kumalizika rasmi kwa muda wa Rais Kabila. 

Tayari Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ametoa wito kwa wanasiasa wa pande zote mbili kuendeleza majadiliano na kuiepusha nchi yako na machafuko. 

Rais Kabila amekuwa madarakani tangu baba yake, Laurent Kabila, auwawe mwaka 2001. Alichaguliwa mwaka 2006 na kisha mwaka 2011, katika uchaguzi ambao wapinzani walilalamika wizi na uvunjwaji wa haki.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga