Watu 10 wamekufa Sudan Kusini kufuatia shambulizi la gruneti
2 Oktoba 2018Kiasi ya watu kumi wamekufa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya bomu la kurushwa kwa mkono kuripuka katika klabu ya usiku kwenye mji wa Yambio, Sudan Kusini.
Kamishna wa polisi katika mji huo, James Monday Enoka aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba watu sita waliojeruhiwa wako katika hali mbaya na kwamba wamepelekwa katika hospitali ya Juba kwa matibabu zaidi.
Mripuko huo ulitokea Ijumaa iliyopita, wakati mtu mmoja aliporusha bomu la mkono katika ukumbi huo uliokuwa na watu 550 waliokuwa wakicheza densi.
Enoka amesema baada ya shambulizi hilo, waliipata miili ya watu wanne. Amesema idadi ya waliokufa iliongezeka jana hadi kufikia watu 10, huku wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa.
Kamishna huyo wa polisi amesema shambulizi hilo halihusishwi na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo tangu mwaka 2013.
Amesema hicho ni kitendo cha kihalifu na mhusika atashtakiwa kwa mujibu wa sheria.