1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiKorea Kusini

Watu 179 waangamia katika ajali ya ndege Korea Kusini

29 Desemba 2024

Idadi ya watu waliofariki kwenye ajali ya ndege iliyotokea mapema Jumapili nchini Korea Kusini imefika 179.

https://p.dw.com/p/4ofQb
Uwanja wa kimataifa wa ndege Muan, Korea Kusini | Ajali ya ndege
Watu wawili ndio wameokolewa kati ya jumla ya 181 waliokuwa kwenye ndege iliyoanguka Muan Korea Kusini Disemba 29, 2024Picha: JUNG YEON-JE/AFP

Hayo ni kulingana na takwimu rasmi ya maafisa wa uokozi ambao wamesema wamefanikiwa kuwaokoa wahudumu wawili.

Ndege hiyo ya abiria aina ya Boeing 737-800, ya shirika la Jeju Air iliwabeba abiria 181 kutoka Thailand kuelekea Korea Kusini.

Ilipata ajali ilipokuwa ikitua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Muan nchini Korea Kusini.

Kulingana na vidio iliyosambazwa mitandaoni iliyonasa tukio hilo, ndege hiyo ilipoteza mwelekeo huku injini zake zikifuka moshi kabla ya kugonga ukuta, kulipuka na kuwaka moto.

Chanzo kamili cha ajali hiyo hakijabainika lakini maafisa wametaja hali mbaya ya hewa na ndege kuingia kwenye injini kuwa huenda zikawa sababu.