1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 40 wauawa katika mapigano Mali

Angela Mdungu
2 Oktoba 2019

Takribani watu 40 wamekufa nchini Mali katika mapigano kati ya wanajeshi wa nchi hiyo na magaidi. Mapigano hayo yametokea katikati mwa Mali

https://p.dw.com/p/3Qewr
Mali Angriff auf das Dogon-Dorf Sobane Da
Picha: Reuters/M. Konate

Serikali ya Mali imesema baada ya majibizano ya risasi, jeshi lilifanikiwa kuidhibiti kambi ya Boulkessi siku ya Jumatatu tarehe 01.10.2019 kwa kushirikiana na Burkina Faso

Kwa mujibu wa kauli iliyotolewa na msemaji wa serikali Yaya Sangare kati ya waliouawa kwenye mapigano hayo ni wanajeshi huku wengine 60 wakiwa hawajulikani walipo. Hii ni baada ya wapiganaji wa kijihadi kushambulia kambi za jeshi katika maeneo ya Boulkessi na Mondoro katika mkoa wa kati wa Mopti.

Kwa mujibu wa mmoja wa walioshuhudia mashambulizi hayo aliyeomba jina lake lihifadhiwe kwa sababu za kiusalama amesema raia wawili ni kati ya majeruhi wa tukio hilo.  Msemaji wa jeshi ameeleza kuwa takribani magaidi 15 waliuawa katika operesheni ya kuwasaka.

Eneo la kati mwa Mali lazidi kulengwa na mashambulizi

Maeneo ya katikati na Kaskazini mwa Mali yamekuwa yakipata mashambulizi na vurugu baada ya kupinduliwa kwa serikali mnamo mwaka 2012. Tangu  wakati huo, makundi ya waasi na badaye kundi la kigaidi la Al Qaeda pamoja na wanamgambo wanaoshirikiana nalo wamekuwa wakishambulia eneo hilo.

Mali militante Bewegung MUJWA
Wanamgambo wa kundi la MUJWA la Mali Picha: Reuters

Wakati huohuo, takribani watu 30 wameuawa mjini Burkina Faso kutokana na machafuko ndani ya wiki mbili zilizopita, wakiwemo 17 waliokufa mwishoni mwa juma. Taarifa hii ni kwa mujibu wa Kamishna mkuu wa mkoa wa Bam Ambrose Ouedraogo. Vurugu  katika manispaa za Bourzanga na Zimtenga hadi sasa zimesababisha watu 19,000 kuyahama makazi yao katika siku tatu zilizopita.

Operesheni za kijeshi  za Ufaransa na Afrika pamoja na juhudi za jeshi la mali, wanamgambo waliotawanyika na operesheni za kijeshi, zinaendelea katika baadhi ya maeneo licha ya kutiwa sahihi kwa makubaliano kadhaa ya amani.