1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 47 wauawa wakimpinga Kabila

20 Machi 2018

Ripoti mpya wa Umoja wa Mataifa inasema ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya waandamanaji wanaopinga utawala wa Rais Joseph Kabila umesababisha vifo vya takribani watu 47. 

https://p.dw.com/p/2ucYp
DRK Protest in Goma, Ostkongo
Maandamano ya kumpinga rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya CongoPicha: DW/J. Vagheni

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema kati ya tarehe 1 Januari mwaka jana na tarehe 31 Januari mwaka huu, watu wasiopungua 47 waliuawa na maafisa wa usalama wakati wa maandamano na kuongeza kuwa kulikuwa na jaribio la vyombo vya dola kufunika ukweli kuhusu vifo hivyo kwa kuiondoa miili ya waliouawa na kuhujumu uchunguzi wa waangalizi wa Congo na wa kimataifa.

Ripoti ya Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa na Mjumbe wa Umoja huo kwa Congo, Zeid Ra'ad Al Hussein, na pamoja na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, Leila Zerrugui, imeonesha mauwaji na matukio mengine mabaya ya ukiukwaji wa haki za binaadamu, yaliyotokana na utumiaji wa nguvu za kupita kiasi kulikofanywa na vikosi vya usalama na ulinzi dhidi ya waandamanaji.

Zaidi ya watoto milioni 4 wana Utapiamlo

Demokratische Republik Kongo Kämpfe zwischen Volksgruppen
Hali ya wakimbizi kwa wanawake na watoto DRCPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Akizungumzia hali jumla ya kiutu nchini DRC, Mark Lowcock, ambae ni mratibu wa misaada ya kiutu katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema "Kuna mahitaji ya kibinaadamu ambayo yamesababishwa na mgogoro wa ndani ambao umeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka uliopita. Watu milioni 13 wanahitaji msaada wa kiutu. Zaidi ya watoto milioni 4.6 wapo katika hali mbaya ya ugonjwa wa utapiamlo wakati wengine milioni 2.2 wako katika hali mbaya zaidi ya ugonjwa ho."

Umoja wa Mataifa umelaani ukandamizaji unaoratibiwa na vyombo vya dola, ukiwemo wa kutumia nguvu isiyo ya kawaida, jambo ambalo linakiuka vikali sheria za kimataifa za ulinzi wa haki za binaadamu na hata katiba ya  Congo yenyewe. Chombo hicho cha kimataifa kimetaka uwepo wa uchunguzi huru wa kimahakama kwa vitendo vyote vya ukiukwaji na tuhuma nyingine, zingatio likiwa vikosi vya ulinzi vilivyoonekana kufanya vitendo hivyo kwa ukatili wa wazi kabisa.

Zerrougui na Zeid wameitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutoa ridhaa ya watu kufanya mikutano na kueleza hisia zao, wakionya ukandamizaji utazusha machafuko zaidi na kusababisha hali ya hatari katika mchakato wa uchaguzi.

Maandamano dhidi ya Rais Kabila yasababisha vifo vya watu 47

Maandamano yalianza kushika kasi nchini humo miezi kadhaa iliyopita na hasa baada ya Rais Kabila kukaidi kuondoka madarakani baada ya muda wake wa kuwa madarakani kufikia mwisho Desemba 2016. Maandamano yaliyofanywa baada ya uchunguzi huu yameshuhudia vifo vya watu wengine 17.

Kanisa nchini Congo linamtaka Rais Kabila akae kando, katika uchaguzi ambao umepangwa tena kufanyika Desemba 23. Ripoti hiyo imehitimishwa kwa kusema "ili kuwepo uchaguzi huru na wa kuaminika tarehe 23 mwezi Desemba, serikali ina wajibu wa kuhakikisha haki za kiraia na kisiasa zinaheshimiwa."

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef