1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu saba wauawa katika mashambulizi ya Urusi Kherson

13 Agosti 2023

Watu saba wameuawa leo katika mashambulizi ya Urusi katika mkoa wa kusini mwa Ukraine wa Kherson. Mashambulizi hayo ya makombora katika kijiji cha Shiroka Balka, ukingoni mwa Mto wa Dnieper yaliiuwa familia nzima

https://p.dw.com/p/4V7K1
Ukraine | Angriff auf Cherson
Picha: via REUTERS

Watu saba wameuawa leo katika mashambulizi ya Urusi katika mkoa wa kusini mwa Ukraine wa Kherson. Wizara ya mambo ya ndani imesema mashambulizi hayo ya makombora katika kijiji cha Shiroka Balka, ukingoni mwa Mto wa Dnieper yaliiuwa familia nzima - mume, mke, mtoto mvulana mwenye umri wa miaka 12 na msichana wa siku 23 na mkaazi mwingine.

Soma pia: Urusi yasema imezima shambulio la Ukraine dhidi ya Crimea

Wanaume wawili waliuawa katika kijiji jirani cha Stanislav, ambako mwanamke mmoja pia alijeruhiwa. Shambulizi la mkoa wa Kherson lilifuatia kauli za Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar jana Jumamosi zikijaribu kutuliza uvumi kuwa vikosi vya Ukraine vilitua katika eneo lililokaliwa la ukingo wa mashariki wa Mto Dnieper jimboni Kherson.

Nchini Urusi, maafisa wameripoti leo kuwa mifumo ya ulinzi wa angani imedungua ndege nne zisizoruka na rubani, katika anga ya eneo la Belgorod na moja katika mkoa jirani wa Kursk ambayo yote yanapakana Ukraine. Mashambulizi ya droni ya Ukraine kwenye maeneo ya mipakani ya Urusi ni matukio yanayotokea mara kwa mara.