1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wa Sidama wapiga kura kuamua mamlaka yao

20 Novemba 2019

Watu wa jamii ya Sidama nchini Ethiopia wanapiga kura ya maoni kuamua juu ya mamlaka ya jimbo hilo la kusini, mtihani mkubwa kabisa kwa uongozi wa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia.

https://p.dw.com/p/3TN01
Vijana wa Sidama wakiwa kwenye msururu wa kupiga kura ya maoni juu ya mamlaka ya jimbo lao la kusini mwa Ethiopia tarehe 20 Novemba 2019.
Vijana wa Sidama wakiwa kwenye msururu wa kupiga kura ya maoni juu ya mamlaka ya jimbo lao la kusini mwa Ethiopia tarehe 20 Novemba 2019.Picha: Getty Images/AFP/M. Tewelde

Vituo vilifunguliwa tangu saa 12:00 asubuhi ya Jumatano (20 Novemba) na kuwakuta watu wakiwa tayari wameshapanga misururu mirefu tangu usiku wa manane.

Kwa wengi, hili ni tukio la kihistoria ambalo wamelingojea kwa miaka kadhaa, alisema mpigakura  Alimetu Daniel, akiongeza kwamba jimbo hilo limekuwa likisubiri hatua hiyo kwa zaidi ya karne nzima.

"Nimefika hapa tangu saa nane usiku kupiga kura yangu mapema. Tulikuwa tukiingojea siku hii kwa hamu kubwa kama vile mjamzito anavyoisubiri siku yake ya kujifungua. Namshukuru Mungu kwamba siku hii imefika na ndiyo maana nipo hapa kupiga kura yangu," alisema msichana huyo mwenye umri wa miaka 26.

Kura hii maalum kwa watu wa Sidama inafanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani, na imekuja na wasiwasi wa kurejelewa kwa ghasia za mwezi Julai, ambapo watu 17 waliuawa baada ya serikali kutangaza kuiahirisha kura hii kwa miezi mitano. 

Kura ya machungu ya kihistoria

Vijana wa Sidama wakiwa kwenye msururu wa kupiga kura ya maoni juu ya mamlaka ya jimbo lao la kusini mwa Ethiopia tarehe 20 Novemba 2019.
Vijana wa Sidama wakiwa kwenye msururu wa kupiga kura ya maoni juu ya mamlaka ya jimbo lao la kusini mwa Ethiopia tarehe 20 Novemba 2019.Picha: Getty Images/AFP/M. Tewelde

Watu wa Sidama, ambao ni asilimia nne ya raia milioni 105 wa Ethiopia, wanapiga kura wakikumbuka machungu makubwa ambayo wao na wazee wao wamepitia katika kupigania mamlaka makubwa ya kujitawala kutoka serikali kuu mjini Addis Ababa.

"Nakumbuka nilipokuwa mdogo, jinsi utawala wa kijeshi ulipokuwa ukiwakata vichwa waliopigania jambo hili na kuvitundika vichwa hivyo maeneo ya wazi kama vile sokoni. Miili yao ilitupwa misituni na kamwe hawakuzikwa kwa heshima. Miongoni mwao, nakumbuka, alikuwa ni mjomba wa mama yangu na mume wa dada yangu," alisema Yerusalem Kabiso, mama mwenye umri wa miaka 48.

Hata hivyo, kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed, kura ya leo ni kielelezo cha njia mpya ya kidemokrasia ambayo utawala wake imeamua kuichukuwa kuelekea Ethiopia yenye maendeleo zaidi. Ametoa wito wa utulivu kwa raia wote.

Mageuzi makubwa aliyoyafanya tangu achukuwe madaraka mwaka jana yamefungua milango kwa zaidi ya makabila 80 nchini mwake kudai mamlaka makubwa zaidi ya kujiendeshea mambo yao.

Ikiwa kura hii ya maoni itapita kama inavyotazamiwa, Sidama itakuwa na mamlaka ya kudhibiti kodi, elimu, usalama na sheria kwenye serikali yake ya ndani, na hivyo kuwa jimbo la kumi lenye mamlaka kama hayo. 

Watu milioni 2.3 wamejisajili kwa uchaguzi huu kwenye vituo 1,700, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi. Vituo vitafungwa saa 12:00 jioni.

AFP, AP, Reuters