1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Denmark asema Ramadhani ni 'hatari kwetu sote'

21 Mei 2018

Waziri wa Denmark anayefahamika kwa mitazamo yake hasi dhidi ya uhamiaji amewatolea wito Waislamu kupumzika wakati wa Ramadhani akisema kufunga ni "hatari kwetu sote".

https://p.dw.com/p/2y3wx
Inger Stojberg
Waziri wa uhamiaji na utangamano wa Denmark Inger Stojberg.Picha: picture alliance/dpa/W. Dabkowski

Matamshi hayo kutoka kwa waziri uhamiaji na utangamano Inger Stojberg, mwanachama wa chama cha mrengo wa kati wa kulia cha Kiliberali, yanakuja baada ya kuanza wiki iliyopita, kwa mfungo wa Ramadhani, ambao ni mwezi ambamo Waislamu duniani kote wanafunga kuanzia alfajiri hadi jua linapozama.

"Natoa wito kwa Waislamu kuchukuwa likizo wakati wa Ramadhani ili kuepusha madhara kwa jamii nyingine ya Denmark," Stojberg aliandika katika makala ya gazeti la udaku la BT.

"Nashangaa iwapo amri ya kidini inayoagiza kutekeleza nguzo ya miaka 1,400 ya Uislamu inawiana na jamii na soko la ajira tuliyonayo nchini Denmark mwaka 2018."

Alisema pia kwamba anahofia kufunga kunaweza kuathiri "usalama na uzalishaji," akitolea mfano wa madereva wa basi wanaoshinda "bila kunywa au kula chochote kwa zaidi ya saa 10." "Hii ni hatari kwetu sote," alisema.

Inger Støjberg
Waziri Inger Stojberg anajulikana kwa mitazamo yake hasi kuelekea uhamiaji.Picha: picture-alliance/dpa/T. Eisenkrätzer

Stojberg aliwahi kuzua utata mwaka uliopita alipoweka kwenye ukurasa wake wa Facebook, picha yake akiwa anatabasamu huku amebeba keki kusherehekea hatua ya 50 ya Denmark kukaza sheria za uhamiaji.

Moja ya hatua kali zaidi ilianza kutekelezwa mwaka 2016, ambayo iliwaruhusu askari polisi kuwanyang'anya wakimbizi vitu vyao vya thamani, ingawa miongozo ya serikali iliziondoa pete za uchumba na harusi, baada ya  hatua hiyo kusababisha hasira na kulinganishwa na Ujerumani ya Wanazi.

Stojberg pia alikosolewa kwa kuanzishwa matangazo kadhaa katika magazeti ya nchini Lebanon mwaka 2015, akiwaonya wanaopanga kutafuta hifadhi ya ukimbizi, juu ya ugumu uliopo katika mchakato wa kutafuta hifadhi nchini Denmark.

Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, nchi hiyo imeimarisha sera zake kuhusu uhamiaji, ikisisitiza kuwa wahamiaji laazima wajifunze kwanza tamaduni za taifa hilo na lugha ili kutangamana katika soko la ajira.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef