Waziri wa Kongo kueleza mbona aliwarudisha nyumbani mabalozi
16 Desemba 2019Waziri wa Kongo wa mambo ya nje ametakiwa kujieleza kwenye baraza la seneti kufuatia hatua yake ya kuwarejesha nyumbani pasipo maelezo yeyote mabalozi wawili wa Kongo. Maseneta wamelezea hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa katiba. Duru kwenye wizara ya mambo ya nje zimelezea kuwa hatua hiyo inatokana na shinikizo la marekani kwa rais Tshisekedi kufuatia hatua ya Kongo kuiunga mkono China kwenye tume ya haki za binadamu mjini Geneva na huko kwenye baraza la usalama mjini New York.
Marie Ntumba Nzenza , waziri wa mambo ya nje wa Kongo, ametakiwa kutoa maelezo ya hatua yake mnamo kipindi cha wiki mbili. Francine Muyumba,kiongozi wa tume ya maswala ya nje kwenye seneti ya Kongo amesema kwamba kikatiba waziri wa mambo ya nje hana mamlaka ya kuteuwa ama kumfuta kazi balozi wa Kongo.
Kwenye barua yake ya kuwafuta kazi mabalozi wa Kongo mjini Newyork na Geneva ,bibi Marie Ntumba Nzeza hakutoa maelezo yeyote bali kuwataka pamoja na familia zao kurejea haraka nyumbani. Ignace Gata balozi wa Kongo kwenye umoja wa mataifa toka mwaka wa 2012, na Zenon Mukongo balozi wa Kongo mjini Geneva (Uswisi) toka mwaka wa 2016 wameachishwa kazi huku umoja wa mataifa ukitarajiwa kuongeza mwishoni mwa mwezi huu, muhula wa kikosi chake nchini, MONUSCO.
Duru Zinaelezea kwamba kuachishwa kazi kwa mabalozi hao kunafuatia shinikizo la Marekani kwa rais wa Kongo Felix Tshisekedi,baada ya mabalozi hao kuuiunga mkono China kuhusu swala la raia wake wa Ouighour kwenye jimbo la Xijiang.
Seneta Francine Muyumba amesema kwamba maswala ya aina hiyo ni mamlaka ya wa Wakongo wenyewe.
Hatua hiyo ya kurejeshwa nyumbani kwa mabalozi hao, imechukuliwa pia dhidi ya balozi wa Kongo nchini Japani. Bin Kithima Ramazani, ametuhumiwa kuuza jengo la ubalozi na kununua lingine pasina kuiarifu serikali ya Kinshasa.
Chama cha FCC cha rais aliestaafu Joseph Kabila kililaani pia hatua hiyo ya kufutwa kazi mabalozi hao. Huku cha UDPS cha rais Tshisekedi kikielezea kwamba hakujakueko na ukiukaji wa sheria katika hatua hiyo ya waziri wa mambo ya nje.