1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wenger ataka Kombe la Dunia kuandaliwa baada ya miaka miwili

3 Septemba 2021

Meneja wa zamani wa Arsenal Arsene Wenger ametoa wito wa kuandaliwa kwa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili, katika mahojiano na jarida la michezo la Ufaransa L'Equipe iliyochapishwa leo Ijumaa.

https://p.dw.com/p/3zreU
UK Arsene Wenger
Picha: Andy Hooper/Daily Mail/SOLO Syndication/picture alliance /

Meneja wa zamani wa Arsenal Arsene Wenger ametoa wito wa kuandaliwa kwa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili, katika mahojiano na jarida la michezo la Ufaransa L'Equipe iliyochapishwa leo Ijumaa.

Raia huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 71 ambaye sasa ni mkurugenzi wa maendeleo katika shirikisho la soka duniani FIFA, pia ametaka kuwepo kwa kipindi kimoja tu cha mechi za kimataifa za kufuzu katika kalenda ya soka duniani.

"Lazima kuwe na mpangilio wa kalenda ya soka ili kusiwe na muingiliano zaidi kati ya mechi za klabu na mechi za kimataifa, na hivyo kuwepo kwa safari chache za wachezaji kujiunga na timu zao za taifa" ameongeza.

Wenger amesema anapendelea kuona dirisha moja tu la kimataifa, labda mnamo mwezi Oktoba, na mechi chache za kimataifa.

"Kwa wachezaji, hakutakuwa na mechi zaidi na kutakuwepo kwa mapumziko ya lazima baada ya mechi za mwisho za kimataifa, angalau kwa siku 25" amesema Wenger ambaye anahisi kuwa mfumo huo alioupendekeza unafaa kuanza kutumika mwaka 2028, miaka miwili baada ya kombe la dunia la mwaka 2026 litakaoandaliwa Amerika ya Kaskazini na Mexico.

"Kile watu wanachohitaji ni soka lenye viwango vya juu, mashindano ambayo ni rahisi kuyaelewa," ameongeza na kusisitiza kuwa hakuna nia yoyote ya kifedha kuhusu pendekezo lake.

Kombe la Dunia la FIFA hushindaniwa na nchi wanachama wa FIFa na huandaliwa kila baada ya miaka minne. Mashindano yajayo yataandaliwa mwaka 2022 nchini Qatar.