1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO kukutana kwa dharura kuijadili Corona

30 Januari 2020

Shirika la afya la ulimwenguni, WHO litaitisha kikao cha wataalamu kujadiliana iwapo wanaweza kutangaza mripuko wa virusi vya Corona kuwa janga la dunia.

https://p.dw.com/p/3Wzzp
Schweiz Hauptsitz der Weltgesundheitsorganisation (WHO) in Genf
Picha: picture-alliance/Xinhua/L. Qu

Shirika la afya la ulimwenguni, WHO kwa mara nyingine linataraji kuitisha kikao cha kamati yake ya wataalamu baadae hii leo ili kujadiliana kuhusu iwapo wanaweza kutangaza mripuko wa virusi vyaCorona kama dharura ya afya duniani.

Virusi hivyo tayari vimeshawaua watu zaidi ya 160 na zaidi ya watu 7, 711 wameambukizwa tangu kulipotambuliwa mgonjwa wa kwanza katika jiji la Wuhan nchini China, Disemba 31.

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Gebreyesus, aliyerejea kutoka China amesema ilikuwa ni muhimu kuitisha mkutano mwingine, ambao ni wa tatu kwa wiki hii kwa kuwa virusi hivyo vimekwishasambaa hadi nje ya China, akisema ni hali inayozidi kutia wasiwasi.

Nchi wanachama wa timu hiyo ya WHO iliamua wiki iliyopita kwamba janga hilo lilikuwa bado halijafikia kiwango cha kutangazwa dharura ya dunia. Hatua kama hiyo ilitangazwa na WHO wakati wa mripuko wa Ebola na mafua ya ndege.

Kulingana na shirika la habari la DPA, chanjo dhidi ya virusi hivyo inaweza kuchukua angalau mwaka mmoja hadi kukamilika kwake, hii ikiwa ni kulingana na muungano wa chanjo, GAVI.

Maafisa wa nchini China wamesema idadi ya visa vipya vya maambukizi vimepanda na kufikia 571 na kufanya jumla ya visa hivyo kufikia 7,700 na watu 170 wamekwishafariki hadi kufikia mapema leo.