1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yasema mtu hujiua kila sekunde 40

10 Septemba 2019

Shirika la Afya Duniani WHO limesema karibu watu 800,000 hujiua kila mwaka -- idadi hii ikiwa ni zaidi ya watu wanaouawa katika vita na mauaji yanayofanywa na mtu dhidi ya mwingine au saratani ya matiti.

https://p.dw.com/p/3PKlt
Selbstmordwelle erschüttert Italien und Griechenland
Picha: Reuters

Katika ripoti yake mpya, shirika hilo la afya duniani limesema viwango vya kujiua duniani vimepungua kwa kiasi fulani kati ya mwaka 2010 na 2016, lakini idadi ya vifo imeendelea kuwa pale kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema katika taarifa kuwa licha ya hatua zilizopigwa, kuna mtu anafariki kila sekunde 40 kutokana na kujiua.

Data za mwaka 2016, ambao ndiyo wa mwisho kutolewa kwa takwimu za vifo vinavyotokana na kujiua, zilionyesha kuwa kwa kila watu 100,000 kulikuwa na vifo 10.5 vinavyotokana na kujiua.

Kwa ujumla viwango vya kujiua duniani vilipungua kwa karibu asilimia 10 kuanzia 2010 hadi 2016, lakini kanda ya Amerika ilionesha kuongezeka kwa viwnago hivyo kwa asilimia 6 katika kipidi cha miaka sita.

Tedros Adhanom Ghebreyesus ehem. Außenminister Äthiopien
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghbereyesus (katika) akizugumza kwenye kikao cha shirika hilo.Picha: DW/T. Woldeyes

Mtaalamu kutoka kitengo cha afya ya akili cha WHO Alexander Fleischmann, amemesema mauaji ya kijiua ni tatizo kubwa la afya ya jamii, na kutoa wito wa hatua kuchukuliwa kushughulikia tatizo hilo.

"Ni muhimu wakati wote katika kuzuwia vifo vya kujiua, kwamba tunawasikilia watu wanaotuzunguka. Tunapaswa kuchukuliwa kwa uzito mtu anaposema hataki tena kuishi au hata wanaposema kwa uthabiti kwamba wanata kujitoa uhai wao. Kila moja wetu ana jukumu katika kuzuwia mauaji ya kujiua. Hivyo sote tunaweza kujitolea kuwasikiliza watu wanaotuzunguka wanapokuwa kwenye huzuni au wanataka msaada wetu."

Wito kwa serikali zaidi kubuni mikakati ya kuzuwia vifo vya kujiua

Ripoti hiyo ya WHO inasema idadi ya mataifa yaliyo na mikakati ya kuzuwia watu kujiua imeongezeka katika kipindi cha miaka mitano tangu kuchapishwa kwa ripoti ya kwanza ya dunia ya WHO. Lakini idadi jumla ya mataifa yaliyo na mikakati hiyo, ambayo ni 38, bado ni ndogo sana na kuongeza kuwa serikali zinahitaji kujifunga kuanzisha mikakati hiyo.

Kujiua kulishika nafasi ya pili kusababisha vifo vingi miongini mwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-29 baada ya majeraha yanayotokana na ajali za barabarani. Mbinu zinazotumiwa zaidi katika kujiua ni pamoja na kujinyonga, kujipiga risasi na, hususani katika maeneo ya vijini, kunywa dawa za sumu za kuulia wadudu.

190905 Infografik Selbstmorde weltweit EN
Ramani ya dunia ikionesha mataifa na viwango vya mauaji ya kujiua duniani.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mauaji zaidi yanatokea katika mataifa maskini na yale maendeleo ya kati, ambako idadi kubwa ya wakaazi wa dunia wanaishi, lakini viwango ni vikubwa zaidi katika mataifa tajiri.

Baada ya Guyana, Urusi ilikuwa ya pili kwa idadi kubwa ya watu wanaojiua. Mataifa mengine yalioko kwenye orodha hiyo ni pamoja na Lithuania, Lesotho, Uganda, Sri Lanka, Korea Kusini, India na Japan, pamoja na Marekani.

Na karibu katika kila taifa, wanaume wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujiua kuliko wanawake. Ni katika mataifa matano tu ya Bangladesh, China, Lesotho, Morocco na Myanmar ambako wanawake zaidi wanajiua kuliko wanaume.

Vyanzo: Mashirika