1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya 20 wauawa Burundi

19 Septemba 2011

Zaidi ya watu 25 wameuawa usiku wa kuamkia leo katika shambulio lililofanywa na watu waliokuwa na silaha dhidi ya baa moja iliyoko katika tarafa ya Gatumba kwenye mpaka wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/12bqy
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais Pierre Nkurunziza wa BurundiPicha: picture alliance / dpa

Ilikuwa ni saa 2.00 za usiku katika baa ijulikanayo Les Amis (Marafiki) katika Zoni ya Gatumba, mkoa wa Bujumbura Vijijini, kwenye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, umbali wa kilomita 15 tu magharibi mwa jiji la Bujumbura, pale kundi la watu waliokuwa wamevalia sare za jeshi na wengine za polisi wakibeba silaha, walipovamia baa hilo na kuanza kufyatuwa risasi na kuripuwa mabomu ya kutupa kwa mkono.

“Ilikuwa kama moto uliowashwa ndani ya baa hilo“, alisema mmoja ya mashahidi. Shambulio hilo liliwauwawa watu wengi ambapo 22 walikufa papo hapo, akiwemo mmliki wa baa hiyo. Wengine 6 walifariki baada ya kufikishwa kwenye hospitali ya Prince Regent Charles, na wengine wawili wameiaga dunia wakiwa kwenye hospitali ya Mfalme Khaled. Wengine wawili wamekufa asubuhi hii. Idadi ya waliokufaa yaweza kuzidi, kwani wengi ya majeruhi waliyolazwa katika hospitali mbali mbali za mji mkuu Bujumbura wako katika hali mahtuti.

Kwa ujumla, majonzi ni makubwa kwa waliopoteza ndugu na jamaa katika shambuliyo hilo. Mwanamke mmoja amempoteza mume wake waliofunga pingu za maisha miezi mitatu tu iliyopita.

Hadi wakati huu, maiti 22 bado zimesaliya kwenye eneo la tukio hilo, miongoni mwa waliouwawa ni wachezaji wawili wa timu ya Espoir na mashabiki wao wawili, waliokuwa wamekwenda kustarehe katika baa hiyo. Mchezaji mwengine wa timu ya Prince Louis amejeruhiwa vibaya, ambapo mkono wake mmoja umekatika kwa risasi.

Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Burundi, Pierre Nkurunziza, amelitembeleya eneo la tukio hilo, kutoa salam za rambirambi kwa waliopoteza watu wao.

Eneo la Gatumba lililoko katika mkoa wa Bujumbura Vijijini, limekuwa ngome ya wapiganaji zamani wa FNL ya Agathon Rwasa, na mara kwa mara limekuwa lilikabiliwa na matukio ya mauaji makubwa.

Shambulio hili la leo limetokea wakati wanasiasa nchini Burundi wakizidi kutafautiana juu ya kuwepo na uasi mpya nchini humo. Vyama vya upinzani vinadai dalili zilizopo ni kuwa bado wapo wapiganaji wapya nchini Burundi na kuitaka serikali kukiri majadilianao ya kisiasa, huku serikali kwa upande wake ikisema waliyopo ni wahalifu waliobeba silaha wanao takiwa kupigwa vita.

Ripoti: Hamida Issa

Mhariri: Josephat Charo