1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky awatembelea wanajeshi karibu na Bakhmut

Sylvia Mwehozi
29 Julai 2023

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameyatembelea maeneo ambayo wanajeshi wake wa vikosi maalumu wamefanikiwa kusonga mbele, karibu na uwanja wa mapambano katika mji wa Bakhmut.

https://p.dw.com/p/4UXZ6
Ukraine
Askari wa Ukraine katika uwanja wa mapambanoPicha: 3rd Assault Brigade/ Ukrainian Armed Forces Press Service/REUTERS

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameyatembelea maeneo ambayo wanajeshi wake wa vikosi maalumu wamefanikiwa kusonga mbele, karibu na uwanja wa mapambano katika mji wa Bakhmut. Zelensky amefanya ziara hiyo wakati Ukraine ikijaribu kuongeza kasi katika kujibu mashambulizi ya Urusi.

Kupitia ukurasa wake wa Telegram, Zelensky aliwapongeza wapiganaji wake kwa ushupavu, na kusifu utendaji wao aliouita wa kishujaa.

Mwezi uliopita, Ukraine ilianza kujibu mashambulizi dhidi ya Urusi, baada ya kujikusanyia silaha kutoka mataifa ya magharibi na kuvisuka vikosi vyake vya mashambulizi.

Licha ya hatua hiyo Ukraine imekiri kukabiliwa bado na mapambano makali na kuitaka Marekani na washirika waipatie silaha za masafa mrefu na mizinga. Mamlaka za nchi hiyo zinadai kwamba vikosi vyake vinapiga hatua taratibu kuelekea karibu na mji wa mashariki wa Bakhmut ambao ulidhibitiwa na Urusi mwezi Mei.