Rais Zelenskyy atembelea wanajeshi uwanja wa vita
4 Oktoba 2023Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametembelea wanajeshi wa taifa lake karibu na uwanja wa vita huko mashariki, ambapo vikosi vya Urusi vimekuwa vikitoa upinzani mkali kwa askari hao baada ya maeneo hayo kurejeshwa tena katika udhibiti wa Ukraine.
Zelenskyy amesema amefanya majadiliano na makanda wa vita katika eneo hilo yalojikita katika masuala ya wakati huo na mahitaji yao.
Kiongozi huyo wa Ukraine pia alisema amekagua silaha zinazotolewa na mataifa ya kigeni, ikiwa ni pamoja na vifaru 2 aina ya Leopard vilivyotengenezwa Ujerumani.
Duru nyingine zinasema Ukraine imefanikiwa kudungua ndege zote zisizo na rubani isipokuwa tatu kati ya zaidi ya 30 zilizorushwa na vikosi vya Urusi kutoka eneo linalokaliwa la Crimea. Serikali ya Kyiv imesema ndege hizo zimetengenezwa Iran.