Ziara ya kwanza ya rais wa DRCongo Tshisekedi Ubeligiji
17 Septemba 2019Felix Tshisekedi ameshafika ziarani April iliyopita mjini Washington ambako alikutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo.
Lakini ziara yake hii nchini Ubeligiji ni ya kwanza barani Ulaya tangu alipotangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais decemba 30 mwaka 2018 katika jamahuri ya kidemokrasi ya Congo.
Awamu rasmi ya ziara hiyo iliyoanza jumatatu usiku, inaanza jumanne hii ambapo rais Tshisekedi na mkewe wamealikwa karamu ya chakula cha mchana pamoja na mfalme Philippe na mkewe malkia Mathilde kabla ya kuhutubia viongozi wa shirikisho la wanaviwanda wa Ubeligiji mjini Brussels.
Jumatano rais Tshisekedi atautembelea mji wa kaskazini wa Anvers ambako amepangiwa kukutana na wakuu wa viwanda vya almasi.
Alkhamisi amepangiwa pia kukutana na mwenyekiti anaemaliza mhula wake wa Halm ashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean Claude Juncker.
Ubeligiji na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo zadhamiria kurejesha uhusiano wa kawaida
Kwa maoni ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubeligiji, Diedier Reyndres aliyempokea rais Tshisekedi alipowasili jumatatu usiku katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Melsbroek, karibu na Brussels, ziara hii imelengwa kusawazisha "hatua baada ya hatua" uhusiano uliopooza tangu mwaka 2015 kutokana na kiu cha rais wa zamani Joseph Kabila cha kutaka kugombea mhula wa tatu hadi alipoamua hatimae Agosti mwaka 2018 kutogombea tena wadhifa huo, uamuzi uliosifiwa wakati ule na Ubeligiji.
Lakini miezi kadhaa ilipita kabla ya watawala hao wa zamani wa Ukoloni kuyatambua matokeo yaliyobishwa ya uchaguzi ambapo chama cha Kabila kinadhibiti wingi wa viti bungeni na wafuasi wake wanashikilia nyadhifa muhimu serikalini."Tunatambua kwamba uhusiano kati ya nchi zetu umekumbwa na misuko suko, tutajaribu kuurekebisha hatua baada ya hatua na bila ya pupa" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubeligiji Didier Reynders katika mahojiano na gazeti la La Libre Beligique.
Kwa upande wake rais Tshisekedi amesema anataraji ziara hii itasaidia kuanzishwa upya ushirikiano wa kijeshi na ahadi za misaada ili kuimarisha mifumo ya afya na elimu nchini mwake.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri-Yusuf Saumu