1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 80 wameokolewa

20 Novemba 2015

Vikosi maalum vya Mali vimeivamia na kuizingira hoteli ya kifahari ya Radisson Blu ya mjini Bamako na kuwaokoa kiasi ya watu 80 waliokuwa wanashikiliwa mateka, baada ya hoteli hiyo kutekwa nyara na watu wenye silaha.

https://p.dw.com/p/1H9eq
Vikosi vya usalama vya Mali vikiwaondoa watu kwenye hoteli hiyo
Vikosi vya usalama vya Mali vikiwaondoa watu kwenye hoteli hiyoPicha: H. Kouyate/AFP/Getty Images

Watu wenye silaha wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu waliivamia na kuiteka nyara hoteli hiyo yenye vyumba 190 na kuwashikilia mateka kiasi ya wageni 170 kutoka mataifa mbalimbali duniani pamoja na wafanyakazi 30 wa hoteli hiyo.

Watu walioshuhudia wanasema watu wapatao 12 wakiwa na silaha waliivamia hoteli hiyo, huku duru za kiusalama za Mali, zikieleza kuwa washambuliaji hao wa jihadi walikuwa wawili au watatu. Msemaji wa wizara ya usalama, amesema milio ya risasi ilisikika katika hoteli hiyo iliyoko katikati ya mji mkuu wa Mali, Bamako na kwamba watu watatu waliokuwa wanashikiliwa mateka, wameuawa katika tukio hilo.

Waziri wa Usalama wa Mali, Salif Traore, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa vikosi maalum vimefanikiwa kuwaokoa mateka kadhaa na wengine 30 walifanikiwa kutoroka wenyewe. Watu walioshuhudia wamesema washambuliaji bado wako ndani na wamechimba katika ghorofa ya saba, na milio ya risasi imekuwa ikisikika mara kwa mara.

Mali Geiselnahme Radisson Blu Hotel in Bamako
Hoteli ya Radisson Blu, BamakoPicha: picture-alliance/dpa

Hoteli hiyo ya Radisson Blu imesema wageni 124 na wafanyakazi 13 bado wako ndani ya hoteli hiyo. Afisa wa usalama amesema awali baadhi ya mateka waliachiwa huru baada ya kuikiri imani yao ya Kiislamu kwa kusoma aya za Koran.

Raia wa Ujerumani waokolewa

Raia wawili wa Ujerumani ni miongoni mwa watu waliookolewa na vikosi maalum vya Mali. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ameyasema hayo leo akiwa ziarani barani Afrika. Bado haijajulikana iwapo kuna raia wengine wa Ujerumani walioko ndani ya hoteli hiyo.

Ufaransa imesema wafanyakazi 12 wa shirika la ndege la Ufaransa waliokuwa wanaishi ndani ya hoteli hiyo, wako salama. Safari zote za ndege za shirika hilo kwenda Bamako, zimefutwa.

Polisi wa Bamako wakiimarisha ulinzi
Polisi wa Bamako wakiimarisha ulinziPicha: H. Kouyate/AFP/Getty Images

Marekani imesema raia wake sita waliokuwa wanashikiliwa mateka ndani ya hoteli hiyo, wameokolewa. Kikosi maalum cha Marekani pamoja na vikosi maalum vya Ufaransa viko katika eneo la la hoteli hiyo kuvisaidia vikosi vya Mali kuwaokoa mateka.

Aidha, Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu amesema wafanyakazi watano kati ya saba wa shirika la ndege la Uturuki, wameokolewa kutoka kwenye hoteli hiyo. Amesema bado wanawasiliana na wafanyakazi wengine wawili wa shirika hilo. Taarifa zinaeleza kuwa watu wengine wanaoshikiliwa mateka ni raia wa China, India na Algeria.

Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita amekatisha ziara yake katika nchi jirani ya Chad, alikokuwa ahudhurie mkutano wa kilele wa kikanda.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,AFPE,APE
Mhariri: Yusuf Saumu