Zuma anaongoza katika kuidhinishwa kuwa kiongozi wa ANC.
26 Novemba 2007Cape Town. Zikiwa zimesalia wiki tatu kabla ya wajumbe 4,000 wa chama tawala nchini Afrika kusini cha ANC kumchagua kiongozi wa chama hicho , Jacob Zuma amepata kiasi cha theluthi mbili ya kura katika njia yake kuelekea katika kiti cha utawala wa nchi hiyo mwaka 2009.
Mpinzani wake pekee, katika kinyang’anyiro hicho , mkuu wa nchi hiyo na kiongozi wa sasa wa chama cha ANC Thabo Mbeki , amepata kura 1,000 kufuatia kukamilika maidhinisho katika majimbo tisa ya ANC. Majimbo matano pamoja na chama cha vijana wa ANC tayari yamemuunga mkono Zuma , ambaye alifutwa kazi na Mbeki mwaka 2005 baada ya mshauri wake wa masuala ya fedha kufungwa kwa kudai hongo kwa niaba ya makamu huyo wa rais.
Zuma alifikishwa mahakamani baada ya hapo , lakini madai hayo yaliondolewa kutokana na matatizo ya kiufundi.