1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma ashinikizwa kwa kutumia fedha za umaa

Buwayhid, Yusra9 Februari 2016

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anatarajiwa kulihutubia bunge la nchi hiyo wiki hii, katika mwaka unaozorota kiuchumi huku naye akikabiliana na kesi ya utumizi wa fedha za umaa.

https://p.dw.com/p/1HrvV
Jacob Zuma
Picha: picture-alliance/landov

Usalama umeimarishwa bungeni kabla ya hotuba hiyo ya rais Zuma, baada ya mwaka jana kutokea fujo pale wabunge wa upinzani walipomzuia Zuma asiendelee na hotuba yake bungeni, na hatimaye ililazimika wabunge hao wafukuzwe kwa nguvu. Wakati rais huyo atakapokuwa anazungumza bungeni siku ya Alhamisi-- iwapo wabunge wa upande wa upinzani watampa nafasi ya kufanya hivyo -- waandamanaji wa vuguvugu linalomtaka rais huyo ajiuzulu kwa upande wao wataandamana katika miji kadhaa ya nchi hiyo.

Halikadhalika leo hii katika mji mkuu wa Johannesburg waandamanaji kadhaa wamekusanyika nje ya Mahakama ya Katiba, ambapo majaji wakisikiliza kesi dhidi ya rais Jacob Zuma kuhusu utumiaji wa fedha za umma kwa kujenga nyumba yake binafsi.

Mamia ya wafuasi wa chama cha upinzani cha Wapiganaji wa Uhuru wa Kiuchumi, ama Economic Freedom Fighters EFF, wameandamana katika majia yaliyoizunguka mahakama hiyo huku wakipiga kelele "Lipa fedha zetu" na "Zuma lazima ajiuzulu"

Protestmärschen gegen Präsident Zuma in Südafrika
Maandamano dhidi ya Rais Zuma Afrika KusiniPicha: picture alliance/AA/A. Hendricks

"Tumekuja hapa kuitaka mahakama itekeleza amri yake kama mlinzi wa umma katika namna ambayo inastahili kufanyika, na tuna uhakika kwamba hilo litatokea kwa sababu tuna kesi iliyokuwa na uzito,” alisema naibu rais wa chama hicho Floyd Shivambu.

Ujenzi na upanuzi wa nyumba binafsi ya rais Zuma wenye thamani ya rand milioni 216 sawa na milioni 24 za Kimarekani ni ishara ya madai ya rushwa na ulafi ndani ya serikali inayoongozwa na chama cha African National Congress.

Machafuko ya kijamii yametanda ndani ya taifa hilo la Afrika Kusini kutokana na kushuka kwa kasi ya uchumi, kuwepo kwa idadi kubwa ya ukosefu wa ajira pamoja na tofauti kubwa baina ya umasikini unaowakabili watu weusi ikilinganishwa na utajiri walionao watu weupe wa nchi hiyo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman